Waziri Jafo azindua kiwanda cha bidhaa za Ngozi Kishapu

May, 06 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amezindua kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kunenepeshea mifugo katika Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga leo Mei 06, 2023 ikiwa ni katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia, amekagua lambo la kukusanyia maji, miradi ambayo inatekelezwa kupitia Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais

Akizungumza na wananchi wakati ziara hiyo Dkt. Jafo ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kusema kuwa imeendana na thamani ya fedha iliyotolewa na Serikali.

Amesema kuwa Serikali imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wanakuwa na maisha bora kupitia miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Ndugu zangu wana Kishapu hongereni sana kwa miradi hii na mmezitendelea haki fedha alizozileta hapa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na niwaahidi tutaendelea kuwaunga mkono,” amesisitiza.

Waziri Jafo amesema kuwa mradi wa kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi kitawanufaisha wananchi kwa kupata masoko ya bidhaa zao ambapo lambo linalokarabatiwa litawasaidia kupata maji kwa ajili ya kunywesha mifugo.

Hivyo, amewataka wananchi kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kutumia na kuitunza miradi hiyo ili iwafae huku akisisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti

Aidha, Dkt. Jafo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi jengo la kusindikia alizeti na unga ameelekeza mashine za kuchakata mazao hayo ziwe zimeshapelekekwa katika mradi huo na kufungwa ili ilanze kuhudumia wananchi.

Katika ziara hiyo, amezindua kiwanda kidogo cha kuchakata bidhaa za Ngozi ambacho kimejumuisha ujenzi wa jengo, kuwezesha mashine za kutengeneza bidhaa hizo na kupeleka vijana sita kozi ya miezi sita.

Pia, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kusindikia alizeti na unga katika kituo cha kunenepeshea mifugo na kukagua ukarabati wa lambo la kukusanyia maji ambavyo vyote vina thamani ya sh. Milioni 389.

Amesema Serikali inapeleka miradi kwa wananchi ili kuwasaidia katika kupata fursa za kimaendeleo pamoja licha ya kuwepo kwa changamoto za mabadiliko ya tabiachi zinazochangia ukame.

“Ndugu zangu niwashukuru sana kwa kutekeleza hii miradi na niwaombe tuilinde asitokee mharibifu akaja kuharibu miundombinu tumsimfumbie macho, lakini pia ajenda yetu kuu tutunze mazingira, usipoyatunza na kuyashughulikia mazingira yatakushughulikia”, amesisitiza.

Kutokana na hali hiyo hivyo, Dkt. Jafo amewapongeza viongozi katika wilaya hiyo kwa usimamizi mzuri wa miradi na kuwa wananchi wanaponufaika nayo ni jambo jambo la heri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude ameshukuru Serikali kwa kuwapelekea wananchi wa wilaya hiyo mradi wa EBARR.

Amesema kuwa kuwepo kwa lambo hilo kutasaidia wananchi hao kuepukana na adha ya changamoto ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Kijiji cha kiloleli.

Mhe. Mkude ameongeza kuwa mradi huo utakuwa wa manufaa makubwa kwa wananchi kwani utasaidia kuhifadhi mazingira katika eneo hilo ikiwa ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kulinda mazingira.

Mradi wa EBARR unatekelezwa pia katika Wilaya ya Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kaskazini ‘A’ Unguja (Zanzibar) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia chini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Settings