Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amewataka wananchi waone thamani ya Muungano wetu kutokana na mafanikio hususan kupitia miradi ya maendeleo. Jafo alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kikazi Zanzibar ya kutembelea nakukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa pande zote za Muungano huku akisisitiza umuhimu wa kuwafundisha wanafunzi faida zake. |
Akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Hamad Hassan Chande alikagua miradi mitano katika mikoa mbalimbali ya Unguja Zanzibar ambapo alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni matunda ya Muungano ambao sote tunajivunia.
“Ndugu zangu, wale wanaobeza Muungano wana cha kujifunza kwani Muungano una faida kubwa kwa Watanzania na miongoni mwa faida hizo ujenzi wa miundombinu ikiwemo shule na vituo vya afya,” alisema waziri huyo.
Waziri Jafo aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku akisisitiza kuwa imejipanga kuondoa changamoto 10 za Muungano zilizosalia.
Aidha, aliwataka wasimamizi wa miradi kusimamia kwa umakini fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Muungano ili zilete matokeo mazuri.
“Binafsi nimefarijika sana kutembelea miradi hii na kukuta inatekelezwa kwa ufanisi lakini niwasihi muhakikishe gharama zinazotumika zinawiana na ubora wa miradi hii. Naagiza Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) msimamie majengo haya kwa ukaribu mkizangatie thamani ya fedha,” alisema.
Hata hivyo Waziri Jafo alielekeza uongozi kukamilisha jengo la huduma ya mama na mtoto lililoanza kujengwa na kuachwa kwa kipindi kirefu bila kumalizika pembeni ya kituo cha afya cha Kianga katika Wilaya ya Magharbi Mkoa wa Mjini Magharibi kujengwa upya kwa kutumia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na kukamilika kufikia Oktoba mwaka huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali anayeshughulia Muungano Zanzibar Khalid Bakar Hamran aliwataka wananchi waibue miradi ambayo wana changamoto ili waweze kutatuliwa.
Alisema fedha za TASAF zimeongezeaka kutoka sh. bilioni 12 za awali hadi 21.2 ambazo zitawawezesha kuendelea kutekeleza miradi ya TASAF katika sekta za afya, elimu na maji.
Hamran aliahidi kuwa mradi huo utaendelea kuboresha sekta ya elimu kwa kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na kumbi za kufanyia mitihani katika skuli za sekondari na ofisi za walimu.
Aliahidi kutekeleza agizo la Waziri Jafo la kuchukua hatua ya kukamilisha jengo la mama na mtoto kando ya kituo cha afya cha Kianga ili lianze kuhudumia wananchi.
Miongoni mwa miradi aliyoitembelea ni pamoja na kituo cha afya cha Kianga, Ukumbi wa kufanyia mitihani katika Shule ya Sekondari Fujoni na vyumba vitatu vya madarasa na jengo la utawala katika Skuli ya Sekondari Mahonda Mkoa wa Magharibi. Miradi hiyo inatekelezwa kupitia fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Miradi mingine aliyotembelea ni soko katika eneo la Kinyasini kupitia mradi wa MIVARF na soko la samaki lililokarabatiwa kupitia fedha za mradi wa SWIOFISH katika eneo la Nungwi mkoa wa Kasakazini.