Waziri Jafo awataka maafisa mazingira kusimamia Sheria ya Mazingira

Apr, 18 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza maafisa mazingira katika halmashauri zote kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira katika maeneo yao.

Ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao na mameneja wa kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) jijini Dodoma leo Aprili 18, 2024.

Pia, ameielekeza NEMC kwa kushiriikiana na wadau kuandaa kikao na maafisa mazingira wa halmashauri zote kwa ajili ya kupeana maelekezo ili ajenda ya mazingira ichukue nafasi yake.

Amesema Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imeanishisha wazi kuwa maafisa hao wanapaswa kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa mazingira kwa Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais na NEMC kwa ajili ya ufuatiliaji.

Aidha, kutokana na changamoto mbalimbali za kimazingira hususan kelele na mitetemo, Dkt. Jafo amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuishirikisha Ofisi ya Makamu wa Rais katika upangaji wa miji.

Amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hatua hiyo itasaidia kubaini upangaji bora wa miji hususan katika matumizi ya maeneo husika kuepusha migogoro ya kimazingira.

Halikadhalika, akizungumza na mameneja wa kanda wa NEMC, Waziri Jafo amewahimiza kuongeza kasi ya utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ili mirai iliyokidhi vigezo iweze tekelezwa.

Amesema kuwa si jambo jema kuona wawekezaji hao wanacheleweshewa vyeti ambavyo wameomba kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira ili waanze miradi.

Pamoja na kuwapongeza kwa usimamizi wa sheria katika kanda zao amewataka kukagua shughuli za wawekezaji wa miradi mbalimbali wanaopatiwa vyeti hiyo kama wanafuata sheria.

“Nendeni mkafuatilie kama waliopata vyetu wanatekeleza yale masharti yaliyomo kwenye vyeti hivyo na sio mtu ameweka cheti chake kama kai ya harusi.

“Tunataka kuona taasisi yetu ya NEMC inaendelea kuheshimika kwa kazi nzuri inayofanya hasa katika usimamizi wa mazingira na sisi kwa upande wake tukiwa wasimamizi wa Sera,” amesema.

Amewasisitiza mameneja hao kuwa na utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa uandaaji wa vyeti unavyoendelea na kuwaelekeza wasaidizi wao waongeze kasi ili vitolewe kwa kasi.

Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw.Thobias Mwesiga amesema walifanya operesheni maalumu kufuatilia na kutekeelza maelekezo ya viongozi kubaini wakiukaji wa sheria na kuchukua hatua ili kulinda mazingira.

Amesema kuwa utekelezaji ulifanyik kwa kufanya ukaguzi katika maeneo ya kimikakati na kuchukua hatua ambapo matokeo yalikuwa katika viwanda 89 viwanda 34 vilibainijka kuiuka sheria na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Pia, Dkt. Mwesiga ameongeza kwa kusema kuwa masoko 21 kati ya 88 yalibainika kukiuka sheria na hivyo kuchukuliwa hatua.

Settings