Waziri Jafo atoa tathmini ya Mkutano wa COP26

Nov, 13 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema mafanikio ya Mkutano 26 wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Glasgow nchini Scotland yataadhihirika zaidi pale mambo yaliyojadiliwa yatatekelezwa kwa vitendo.

Jafo amesema hayo leo Novemba 13, 2021 alipozungumza na wanahabari katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mkoani Dar es Salaam wakati akitoa tathmnini ya mkutano huo.

Alitoa wito kwa Watendaji katika Wizara, Taasisi na Sekta binafsi watekeleze majukumu yao katika kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya hatua za kuchukua yanayozihusu Wizara na Taasisi zao katika kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa kuwa Tanzania kupitia Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan Tanzania imeungana na Jumuiya ya kimataifa kupitisha na kutekeleza azimio la kuhifadhi misitu duniani, natoa wito kwa wakuu wa mikoa, wilaya na Halmashauri zote nchini kutekeleza maagizo ya kupanda miti 1,500,000 kila mwaka ili kumuunga mkono na kufanikisha jitihada za kuhimili mabadiliko ya tabianchi,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa miradi ya Kimkakati ya Treni ya Umeme (SGR), Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere na Mradi wa Mabasi yaendayo kasi (BRT) imekuwa ni miradi ya mfano kimataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ametoa wito kwa wananchi kwa ujumla kuunga mkono utekelezaji wa miradi hiyo na watendaji wa taasisi husika kuhakikisha miradi hii inasimamiwa vizuri ili kuwa na matokeo mazuri.

Alivitaka Vyombo vya Habari, taasisi na wadau wote waongeze jitihada za kutoa elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi hususan katika maeneo ya mijini na vijijini ili wananchi waweze kuchukua tahadhari na kutumia mbinu za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali.

Pia alisisitiza Sekta binafsi ishirikiane na Serikali na wadau wengine katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya tabianchi na mikakati ya Serikali ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Alibainisha kuwa Mkutano huo umekuwa muhimu na wa manufaa makubwa kwa Taifahususan katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi hapa nchini na duniani kwa ujumla.

”Katika mkutano huo sisi kama Taifa tumeweza kuwasilisha taarifa na mchango wetu katika kupunguza uzalishaji wa gesi joto zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Tanzania imeungana na mataifa mengine kuwasilisha msimamo wa nchi katika maeneo na hatua mbalimbali za kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi duniani,” alisisitiza Jafo.

Settings