Waziri Jafo atoa siku 7 kwa ghala la kusafirishia kemikali ya salfa kufanya marekebisho

Apr, 09 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa siku saba kwa Kampuni ya African Inland Logistics Ltd. kusimamisha shughuli za usafirishaji na utunzaji wa kemikali ya salfa, katika ghala lake na kulifanyia marekebisho ili kuepusha kuhatarisha afya za wakazi wa eneo hilo.

Ameyasema hayo leo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam katika Kata ya Sandali alipotembelea na kukagua ghala hilo.

“Natoa maelekezo kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamisha shughuli zote za ghala hili mpaka watakapofanya marekebisho katika usafirishaji na uhifadhi wa kemikali hii ya salfa katika ghala hili ambalo liko katika makazi ya watu, tunapenda uwekezaji katika nchi yetu lakini ni lazima kulinda afya za Wananchi. Wahakikishe wanaposafirisha kemikali hii hamna hata punje moja inayomwagika,” alisema.

Aidha Waziri Jafo ameelekeza kampuni hiyo pia kufanya ukaguzi wa mazingira mara moja kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.

“Mnafanya kazi wakati hamna cheti cha aina yoyote, naagiza kufanya kaguzi ya mazingira, tunapenda uwekezaji uende mbele lakini siyo kudhuru wananchi kama hivi mnavyofanya,” alielekeza.

Meneja NEMC Kanda ya Kusini Mashariki Bwana Hamad Taimuru amewataka wenye ghala hilo kutumia mifuko maalumu ya kufungashia kemikali (jumbo bags) ili kuepusha umwagaji hovyo barabarani wa kemikali hiyo ya salfa wakati wa usafirishaji wake kutoka bandarini kwenda kwenye ghala hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Sandali Mhe. Christopher Kabalika amemshukuru Waziri Jafo kwa kutembelea eneo hilo na kujionea hali halisi iliyopo eneo hilo ambapo umwagikaji huo wa kemikali ya salfa unaleta madhara kwa wananchi wa eneo hilo.

Diwani huyo aliahidi kuwa wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kwa uwekezaji lakini kwa madhara ya namna hii hawatakuwa tayari kuvumilia.

Pia, ananchi hao wametoa kero zao mbele ya waziri kwa kulalamika kuhusiana na madhara wanayopata baada ya kemikali hiyo kumwagika katika barabara ambayo ni makazi ya watu.

Mzee Said Elihuruma alidai kuwa wanapitia hali mbaya kwani watoto wao wanaumwa vifua na kukohoa hata watu wazima kuwashwa ngozi na kuvimba hivyo wanamuomba waziri awasaidie katika suala hilo.

ReplyForward
Settings