Waziri Jafo asisitiza matumizi ya nishati mbadala kwa taasisi

Apr, 20 2023

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo amezisisitiza taasisi za umma na binafsi zenye kuhudumia watu zaidi ya 100 zitumie nishati mbadala ili kupunguza kasi ya ukataji wa miti.

Ametoa msisitizo huo Aprili 19, 2023 wakati akizindua Kampeni ya Mazingira na Matumizi ya Nishati Mbadala pamoja na Mashindano ya Upandaji wa Miti katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu wilayani kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi kuungana katika kutunza na kulinda mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoathiri mazingira na uchumi.

“Ndugu zangu lengo kubwa la katazo la matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi ni kusonga mbele katika kudhibiti uharibifu wa mazingira, ukataji miti na maelekezo hayo hayakugusa mwananchi mmoja mmoja licha ya kwamba wananchi wanatakiwa kutunza mazingira na kuacha kukata miti ovyo,“ amesisitiza.

Aidha, Waziri Jafo amepowangeza Taifa Gas kwa kufunga mtungi wa gesi wa katika shule hiyo kwa ajili ya matumizi ya jiko la akisema kuwa taasisi kuacha kutumia kuni na mkaa inawezekana.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kujipambanua katika suala zima la mazingira kwa kutekeleza miradi ya kujali mazingira.

Kwa upande wake Mkuu Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amesema mkoa huo una changamoto kubwa ya kimazingira hivyo wameamua kujipambanua katika upande wa mazingira ili kupambana na hali hiyo.

Amesema Mkoa wa Pwani umeshapanda miti milioni tisa sawa na asilimia 82 na lengo likiwa ni kupanda miti zaidi ya milioni 13 huku akiongeza kuwa wamejipanga kuongeza usimamizi wa mazingira, upandaji miti, teknolojia mbadala na uchumi.

Bi. Angela Bhoke kutoka Taifa Gas ameeleza kuwa wanajenga kiwanda cha mitungi ya gesi katika eneo la Misugusugu lengo ni kushirikiana na Serikali katika kudhibiti uharibifu wa mazingira na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala.

Settings