Waziri Jafo ashukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano

Sep, 08 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Nchi za NORDIC Mhe. Anne Veathe Tvinnereim.

Katika mazungumzo hayo Waziri Jafo alishukuru Norway kwa ushirikiano wake kwa Tanzania hatua iliyochangia maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu na kusema ushirikiano huo uliodumu kwa takriban miaka 55 uendelee.

Alisema uhifadhi wa mazingira unaoonekana ni kutokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inakuwa salama katika sekta ya mazingira.

Dkt. Jafo alisema Serikali ya Tanzania inatarajia kushirikiana na Serikali ya Norway katika usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali zinazopatikana baharini bila kuathiri hifadhi ya mazingira.

Alisema upo mpango kazi wa kuhakikisha mazingira ya bahari yanakuwa salama dhidi ya changamoto ya taka za plastiki ambazo ni hatari kwa maisha ya viumbe wa baharini.

Waziri Jafo alisema eneo lingine kuwa ni kuiwezesha kamati ya kitaifa ya uchumi wa bluu kufanya kazi zake kwa ufanisi sambamba na kuhakikisha upandaji wa mikoko unakuwa endelevu ili kusaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Waziri Tvinnereim amepongeza juhudi za Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais katika kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwani imeweza kuandaa Sera ambazo zinachochea katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Pia waziri huyo aliahidi kuwa Serikali ya Norway iko tayari kuongeza nguvu katika jitihada zinazofanyika hapa nchini ili kufikia malengo ya kuwa na Tanzania inapata matokeo mazuri katika uhifadhi wa mazingira.

Naye Balozi wa Norway nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen alisifu Tanzania kwa jitihada za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikihatarisha usalama wa chakula.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama, Balozi wa Tanzania nchini Norway Mhe.Grace Olotu pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.

Settings