Waziri Jafo apongeza Bahi kwa utekelezaji wa usimamizi wa mazingira

May, 07 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Wilaya ya Bahi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali ya upandaji miti kwa wanafunzi.

Ametoa pongezi hizo leo Machi 7, 2022 wakati aliposhuhudia utiaji saini wa makubaliano ya upandaji miti kati ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi na walimu wakuu wa shule za msingi uliokwenda sambamba na Bonanza la Walimu wilayani humo.

Dkt. Jafo amesema kuwa hatua ya kusaini mkataba huo itaongeza hamasa kwa walimu kuwasimamia wanafunzi katika shule zao kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti.

Alisema tuna kila sababu ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kijani na ndiyo maana Januari 22, 2022 ilizinduliwa kampeni ya utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ‘Soma na Mti’ lengo likiwa ni kuweza kupata miti mingi zaidi sambamba na maelekezo ya Serikali kwa kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5.

“Niwapongeze sana Bahi leo mnasainiana mikataba baina ya Mkuu wa Wilaya na walimu kwa ajili ya kukijanisha Bahi, Dodoma na Tanzania kwa ujumla, licha ya kuwepo kwa jumla ya wilaya 139 na halmashauri 184 ninyi mmeenda sambamba na Kampeni ya Soma na Mti, hakika mmekuwa mfano wa kuigwa,” alisema Dkt. Jafo.

Aidha, Waziri Jafo aliwataka wakuu wa mikoa wengine nchini washushe ajenda hii kwa wakuu wao wa wilaya ili wawaelekeze wakuu wa shule kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira kwa kuiga mfano huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda alisema walimu ni nyenzo muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya utunzaji wa mazingira hivyo ni muhimu kuwatumia.

Alisema walimu wakitumika ipasavyo katika kuwajenga wanafunzi kupenda mazingira na kupanda miti itasaidia shule zetu kupata miti ya kutosha na hivyo nchi yetu itapata mvua.

“Mheshimiwa waziri leo utashuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Mkuu wa Wilaya na walimu wakuu wa shule zote za msingi ili kuhakisha kampeni ya Soma Mti inafanyika kwa vitendo,” alisema Munkunda.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bahi Mhe. Kenneth Nollo alisema utamaduni wa kila mwanafunzi wa kuwa na mti ni jambo zuri kwani itsaidia hata akifikia umri wa mtu mzima akiwa mtu mzima ataona umuhimu wa miti na pia itasaidia kuongeza idadi ya miti nchini.

Katika bonanza hilo pia Waziri Jafo alishiriki katika zoezi la kupanda miti katika viwanja vya Shule Msingi Bahi Sokoni, kutunuku zawadi kwa washindi wa michezo na kufungua mchezo wa mpira wa miguu kwa walimu.

Settings