Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Waziri Jafo amtaka mmiliki machimbo ya vifusi kupata kibali


Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelekeza miliki wa machimbo ya vifusi vya kokoto katika eneo la Mbutu Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam kufanya Tathimini ya Athari Kwa Mazingira.

Ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya ukaguzi wa mazingira katika eneo hilo ambapo ameonesha kutoridhishwa na namna shughuli za uchimbaji zinavyofanyika katika eneo hilo ambazo hazizingatii utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Kutokana na hali hiyo Dkt. Jafo alimtaka mmiliki huyo kufika katika ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kujisajili na kupata cheti cha mazingira ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Alisema wawekezaji wote waliopewa eneo hilo kwa ajili ya uchimbaji wa kifusi lazima wawe na cheti cha kibali cha mazingira ambacho kimesajiliwa katika ofisi za NEMC na kiainishe aina ya kazi itakayofanyika.

Kwa upande wake Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kusini Bw. Hamad Taimuru aliwataka wamiliki wa machimbo hayo kufika katika ofisi za Baraza hilo na kusajili machimbo hayo na kufanya Tathmini ya Athari Kwa Mazingira ili kulinda mazingira na viumbe hai wengine.