Waziri Jafo ahimiza kila mwanafunzi apande mti na kuutunza

Jan, 17 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ameelekeza kila mwanafunzi apande mti, kuusimamia na kuutunza hatua itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo leo Januari 17, 2022 jijini Tanga wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua na kuhamasisha shughuli mbalimbali za hifadhi na utunzaji wa mazingira.

Alisema kuwa upungufu wa miti umekuwa chanzo cha kiwango cha mvua kimepungua na joto limeongezeka kwa kasi hali iliyosababisha ukame ambao matokeo yake baadhi ya wanyama wanakufa.

Kwa mantiki hiyo alisema kuwa kuna umuhimu wa kuwajengea utamaduni wa kupanda miti watoto wa shule ili kuwa na kizazi chenye kujali na kupenda mazingira.

“Pamoja na maelekezo ya Serikali ya Serikali ya kupanda miti milioni moja na nusu kwa kila halmashauri ambayo lengo ni miti milioni 276 kwa halmashauri zote 139 lakini kila mwanafunzi kuanzia chekechekea, msingi, sekondari akipanda mti mmoja na kuusimamia kwa mwaka mzima ndio utakuwa mkombozi wetu kukabiliana na changamoto hizi za kimazingira,” alisema.

Aidha, Waziri Jafo aliwaelekeza viongozi wa mikoa na wilaya kusimamia kikamilifu zoezi la usafi wa mazingira na kusema kuwa ni aibu kwa majiji makubwa kuwa machafu.

Alisisitiza kuwa maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa kuhusu usafi wa mazingira yatekelezwe na usafi katika siku za Jumamosi uwe ni utamaduni na uendelee kushika kasi.

Akitembelea dampo la kisasa la Jiji la Tanga ambapo alionesha kuridhishwa na namna wanavyoshughulikia taka ngumu na kuwapongeza viongozi wanaosimamia dampo hilo.

Hivyo, Waziri huyo aliwataka viongozi wa halmashauri zingine ambazo zimenufaika na miradi ya ujenzi wa madampo ya kisasa kuhakikisha wanayasimamia ipasavyo.

Katika hatua nyingine waziri alifanya ziara katika eneo la Chongoleani ambako kunakotarajiwa kujengwa bandari ya kupokelea mafuta ili kujiridhisha uzingatiaji wa maelekezo ya Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).

Aliwataka wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na watalaamu kutoka Mamlaka ya Bandari kuhakikisha maelekezo ya EIA yanazingatiwa ili mradi huo uwe endelevu na rafi kwa mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi wa Wilaya ya Tanga wa Wakala Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Bi. Bhoke Masisi alisema wakala huo umeotesha miti 75,000 na kutoa wito kwa taasisi kufika na kuchukua miche kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao.


Bi. Masisi alisema miti ina faida nyingi zikiwemo kutoa vivuli na kupunguza mmomonyoko wa udongo huku akitaja mikakati ya TFS ikiwemo kuratibu hewa ya ukaa.

Settings