Waziri Jafo ahamasisha ushirikiano Sensa

Aug, 21 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa Watanzania kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakaowafikia kwa kutoa takwimu sahihi.

Ametoa wito huo leo Agosti 21, 2022 wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza katika Tamasha la Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi katika viwanja vya Shule ya Msingi Chanzige Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Dkt. Jafo aliwahimiza wananchi hao kuwa tayari kuhesabiwa ili Serikali ipate takwimu sahihi za watu na makazi zitakazosaidia katika kupanga mipango yake ya kibajeti ione idadi kamili ya wananchi na hivyo kuwapelekea maendeleo.

“Ndugu zangu jukumu kubwa lenu ni kuwa tayari kuhesabiwa na tuwape ushirikiano makarani na maafisa wote wa sensa kwa maana nyingine tusipowapa ushirikiano sensa hii haitakuwa na maana tena,” alisema.

Alisema maandalizi ya sensa yamekamilika na watendaji wako tayari kuanza zoezi hilo kwa ufanisi kutokana na kuwa litatumia vishkwambi ambavyo vitachukua taarifa na kuituma moja kwa moja kwenye kituo cha kupokelea taarifa.

Aidha, Waziri Jafo alisema ana imani kuwa sensa ya mwaka 2023 imekuwa na hamasa kutoka kwa wananchi kutokana na kutolewa kwa elimu ikilinganishwa na mwaka 2012 ambayo ilikuwa na changamoto katika baadhi ya mikoa ikiwemo Mtwara, Lindi, Tanga, Pwani na Kigoma.

Awali akimkaribisha Waziri Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abuubakar Kunenge alisema sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya mfano kwakuwa itahusisha watu pamoja makazi tofauti na sensa zilizopita ambazo zilichukua takwimu ya watu pekee.

Alisema pia sensa hii itatumia teknolojia ya vishkwambi ambayo itarahisisha ukusanyaji na utumaji wa takwimu kutoka sehemu za makazi zinapochukuliwa na kutumwa panapohusika kwa haraka.

“Ni matarajio yangu zoezi la sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu litakwenda vizuri kwani maeneo mengi yatafikiwa kwa ukamilifu na ili tufanikiwe lazima kuwe na utayari ya wananchi na uwezo wa Serikali katika kuendesha na kusimamia zoezi hili,” alisema Kunenge.

Tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Bi. Zuwena Omary na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson John.

Settings