Wazalishaji wa mifuko mbadala wapewa onyo

Feb, 21 2020

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Zungu amesema katika kipindi hiki cha miezi tisa (9) tangu Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga marufuku mifuko ya Plastiki za mwaka 2019 zianze kutekelezwa, Serikali imefanya jitihada za kutoa elimu kwa wadau mbalimbali, kuandaa viwango vya ubora wa mifuko mbadala ya Non-woven, kufanya kaguzi katika maeneo ya uzalishaji, usambaji na uuzaji wa mifuko mbadala.

Akifungua kikao cha wadau katika ukumbi wa LAPF, Kijitonyama chenye lengo la kukuza uelewa wa Sheria na Utekelezaji wa Kanuni ya Katazo la Mifuko ya Plastiki kwa wazalishaji, waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa mifuko mbadala Jijjini Dar es Salaam, Zungu ameainisha kuwa mifuko mbadala inayoruhusiwa kisheria kutumika kubebea bidhaa hapa nchini ni lazima ikidhi matakwa ya kisheria. “Mwongozo umeainisha viwango vya ubora wa mifuko

mbadala ya “Non-woven” ni uzito usiopungua 70GSM; iwe inayoweza kurejelezwa (recyclable); iwe na anuani ya mzalishaji au nembo ya biashara (trade mark); ionyeshe uwezo wake wa kubeba (carrying capacity); na iwe imethibitishwa ubora wake na Shirika la Viwango-TBS” Zungu alisisitiza.

Waziri Zungu amesema kuwa hadi sasa tani 54 za mifuko aina ya non-Woven zimekamatwa na kusisitiza kuwa hivi sasa adhabu kali zitatolewa ikiwa ni pamoja na faini, kufunga viwanda na kusisitiza kuwa msako mkali unaanza kwa wazalishaji na wasambazaji wa mifuko isiyokidhi viwango. “Katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Juni, mosi 2019 shehena ya mifuko mbadala isiyokidhi viwango isiyopungua tani 54.035, katoni 12,767 na vipisi 11,191, 919 imekamatwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara wakati wa kaguzi na hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na Kanuni zake, zimechukuliwa kwa waliokutwa na makosa. Hatutishani lakini tunatoa tahadhari! Wenye viwanda wanaoendelea kukaidi wakikamatwa watashtakiwa kwa kuhujumu uchumi” Zungu alisisitiza

Settings