Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi hiyo kuendelea kudumisha na kuuenzi Muungano kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, amewataka kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira pamoja na kusimamia vizuri miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ili ilete tija na kuwanufaisha wananchi na walengwa waliokusudiwa.
Mhe. Khamis ametoa wito huo Machi 30, 2023 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa lengo la kupitia Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2023/2024.
Aidha, amewapongeza wafanyakazi hao utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kusisitiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kujituma kwa kuongeza ufanisi kwa ustawi wa Ofisi na Taifa kwa ujumla.
“Ni wajibu wenu ninyi wajumbe na washiriki wote wa Baraza hili kutumia fursa mliyoipata kuhoji na kutoa mapendekezo chanya yatakayokuwa na msaada kwa Ofisi ili hatimaye mchango wa Ofisi ya Makamu wa Rais uonekane katika jitihada za pamoja katika kuiletea nchi yetu maendeleo,“ alilisitiza.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi alisema Mabaraza ya Wafanyakazi mahali pa kazi ni takwa la Kisheria.
Alifafanua kuwa kifungu Na. 30 (3) cha Sheria ya Majadiliano katika Utumishi wa Umma Na. 19 ya mwaka 2003 kifungu cha 73 (1-3) cha Sheria ya Uhusiano Kazini Na.6 ya 2004 na kanuni zake za 2007 vinaelekeza kufanyika kwa mabaraza hayo.
Hivyo, Mitawi alisema Baraza la Wafanyakazi ni muhimu katika kujadili masuala mbalimbali ya wafanyakazi kwa upana kwa kuzingatia haki, weledi na kuibua changamoto za kiutendaji na hatua za kukabiliana nazo.