Wakurugenzi wasimamie upandaji miti kwa wanaojenga nyumba

Aug, 11 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhusisha masharti ya upandaji miti kwa vibali vya ujenzi.

Ametoa maelekezo hayo leo Agosti 11, 2022 wakati akishiriki uzinduzi wa kampeni ya ‘STAMICO na Mazingira At 50’ iliyokwenda sambamba na zoezi la upandaji miti katika eneo la wazi Ipagala jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika eneo hilo mara baada ya matembezi ya hisani, Dkt. Jafo alipongeza Wizara ya Madini na shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika utunzaji wa mazingira.

Alisema ili kuwa na dhamira ya dhati katika utunzaji wa mazingira na kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika zinazoyakabili maeneo mbalimbali nchini wakurugenzi wanapogawa viwanja wahakikishe vinakuwa na eneo la kupanda miti.

“Niwapongeze sana STAMICO kwa kuja na kampeni hii ambayo itatusaidia katika kuifanya Dodoma na mikoa mingine kuwa ya kijani na mnaonesha kuunga mkono juhudi za viongozi wetu wakuu ambao wamekuwa wakituelekeze tutunze mazingira,” alisema.

Dkt. Jafo alipongeza juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali za kupanda miti ambapo kupitia zoezi la upandaji miti milioni 1. 5 kwa kila halmashauri kwa mwaka limeonesha mafanikio kwa kufikia zaidi ya asilimia 80.

Kutokana na hatua hio waziri alihimiza matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajii ya kuni na mkaa na hivyo kupunguza changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha uchumi wa nchi kushuka.

Kwa upande wake Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Doto Biteko alitoa rai kwa STAMICO kuhakikisha kuwa wanaisimamia miti hiyo na kuitunza iweze kuishi kwa miaka mingi zaidi.

Biteko alisema haitakuwa na maana kama tunatumia muda na rasilimali kupanda miti halafu inakufa itakuwa hatutendi haki hivyo tunapaswa kupanda miti mingine.

Pia alimshuruku Waziri Jafo kwa kushiriki katika kampeni ya upandaji miti pamoja na kutoa hamasa kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza kampeni hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse alisema wanatarajia kupanda miti 10,000 na kwa awamu ya kwanza ilipandwa miti 100 kati ya 2,000 itakayopandwa katika jiji la Dodoma na baadaye 8,000 iliyobaki katika mikoa mingine ambako inaendesha miradi yake.

Dkt. Mwasse alisema kuwa lengo kampeni hiyo ni kushiriki kikamilifu katika zoezi la utunzaji wa uoto wa asili na kuleta hamasa ya kutunza mazingira ili shughuli za uchimbaji madini ziwe rafiki kwa mazingira.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Rosemary Senyamule alitoa rai kwa STAMICO kutafuta teknolojia mbadala wa matumizi ya miti katika shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kupunguza ukataji wa miti.

Alisema shughuli za madini ni muhimu na zinapaswa kuwa endelevu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu lakini zinapaswa kuzingatia uhifadhi wa mazingira

Aidha, aliahidi kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kupongeza juhudi zilizofanyika katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa.

Settings