Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Waitara: NEMC hakikisheni miti inapandwa kuzunguka machimbo


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha maeneo ya wachimbaji yanapandwa miti.

Waitara alitoa maelekezo hayo jana baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Buhemba wilayani Butiama mkoani Mara wakidai kuwa miti wanayopanda inakauka.

Akizungumza na wachimbaji hao zaidi ya 300 katika eneo hilo alisema kuwa maeneo hayo yana changamoto ya ukataji miti kwa wingi na hivyo ni lazima kupandwa miti kwa wingi.

Naibu waziri huyo alibainisha kuwa pamoja na jitihada za wananchi kupanda miti lakini inayopandwa inakauka kutokana na kupandwa sehemu zisizo sahihi.

Kwa mantiki hiyo alisema ipo haja kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kutoa ushauri kuhusu miti sahihi inayopaswa kupandwa badala ya kuacha wananchi kupanda miti kiholela matokeo yake inakauka.

“Tunaona mnatumia sana magogo kwa katika shughuli zenu na hiyo husababisha ukataji miti kushamiri sisi tunashauri mtumie miti inayopandwa kibiashara na si miti ya asili kwani ikipotea imepotea haitapatikana mingine,” alisisitiza.

Aidha Waitara ambaye aliambatana na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC Kanda ya Ziwa na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara alisema ipo haja kwa kila kaya kupanda miti angalau mitatu hadi mitano.

Pia alitshauri Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutunga sheria ndogo zinazomtaka kila mwananchi katika ngazi zote kupanda miti katika maeneo yao sanjari na kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha upandaji miti.

“Kama ambavyo Mheshimiwa Makamu wa Rais alivyoelekeza kila wilaya ipande miti, tumuomba kila Mkuu wa wilaya na viongozi wa chini yake watutembeze katika maeneo yao kuona kama zoezi hilo limetekelezwa ipasavyo,” alisema.

Awali akimkaribusha naibu waziri, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anna Rose Nyamubi aliomba kuwekwa utaratibu wa kudhibiti vifusi vilivyochenjuliwa na kurundikwa.

Alisema kuwa baadhi ya wachimbaji wanahamisha vifusi hivyo na kwenda kuchenjua tena katika maeneo mengine hatua ambayo inasababisha kusmbaa hovyo.

Naibu Waziri Waitara yuko katika ziara ya kikazi kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu juhudi za Serikali katika kulinda hifadhi ya mazingira na kuhamasisha usafi wa mazingira.