Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Uchumi wa Bahari kuzingatia hifadhi ya mazingira


Ofisi ya Makamu wa Rais imehakikisha hifadhi endelevu ya mazingira ya pwani ikiwemo mgawanyo wa maeneo ya bahari kwa kila shughuli inayofanyika ndani ya bahari inazingatiwa katika kuelekea Uchumi wa Bahari.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Emelda Teikwa kwenye kikao cha kupitia taarifa ya tathmini ya awali ya Uchumi wa Bahari kilichofanyika Oktoba 5 hadi 6, 2020 jijini Morogoro na kuhusisha wadau ambao sekta zao zinategemea sekta ya bahari, maziwa na mito.

Alibainisha Tanzania ina ukanda wa bahari wenye urefu wa zaidi ya kilometa 1,000 na takriban kilometa 64,000 za eneo la maji ya maziwa na mito ambalo linaweza kutumkia kukuza uchumi.

“Pamoja na mambo mbalimbali lengo la Ofisi la Makamu wa Rais ni kuhakikisha tunapoelekea uchumi wa bahari hifadhi ya mazingira inazingatiwa na ndio maana tunasisitiza mifumo ikolojia ya bahari kwa kuhusisha jamii zinazotumia rasilimali hizo,” alisema.

Aidha, Teikwa aliongeza kuwa taarifa hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Wanyamapori na Mazingira (WWF) inaangalia nini Tanzania ifanye kuelekea uchumi wa bahari na kuboresha sekta hizi ziwe na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na kuhifadhi mazingira.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi unaohusu mambo ya bahari na pwani kutoka WWF, Dkt. Modesta Medard alishukuru Serikali kwa kuhusisha wadau katika suala la uchumi wa bahari.

Pia Dkt. Modesta aliiomba Serikali kuanisha sekta zinazotumia rasilimali ya bahari ili kuweza kuona ni namna gani tutaweza kualika wawekezaji katika sekta hizo.

“Suala la uchumi ‘blue economy’ linagusa wananchi wengi kwa mfano uvuvi, usafirishaji au utalii zikipewa kipaumbele maisha yatabadilika, wakulima wa mwani je watanufaika vipi, lazima tufanye tathmini ya uchimbaji wa gesi na mafuta na kwa kufanya hivyo tutakuza uchumi,” alisema.

Nae Mtaalamu wa Miradi wa Shirika la Mandeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbasi Kitogo alisema kuna changamoto katika uchumi wa bahari kwani kwa kuwa nchi inafaidika kidogo na uchumi wa sekta hii.

Kitogo alisema kuwa taarifa hiyo iliyoandaliwa itawawezesha kuangalia namna gani ya kuboresha na kupata mkakati wa kitaifa ulio thabiti katika kuimarisha sekta hiyo.

“Sisi kama UNDP tunashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na WWF na pia na nchi katika kujenga uwezo wa kitaasisi, kisera na kijamii katika kuhakikisha rasilimali hizi zinatumika inavyotakiwa,” alisema.