Tanzania imeweka msisitizo kwa nchi za Afrika kuungana na kuhakikisha uhifadhi wa mazingira unakuwa endelevu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe wakati akifungua Mkutano wa Kundi la Majadiliano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (AGN) kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni jijini Dar es Salaam leo Agosti 07, 2025.
Prof. Msoffe amesema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa wadau wote wa mazingira kuguswa na kupaza sauti ili kuokoa sekta hiyo kutoka kwenye changamoto za uharibifu wa namna yoyote ile.
Alisema katika mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 60 utakuwa na kazi ya kupokea taarifa ya mijadala mbalimbali ili kuwa na sauti moja kwa lengo la kuwakilisha maslahi ya Bara la Afrika katika mazungumzo ya kimataifa ya mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe alibainisha kuwa kuanzishwa kwa Sekretarieti ya AGN ni hatua muhimu kwani itahakikisha kila nchi ya Kiafrika, inapata utaalamu katika masuala ya hifadhi ya mazingira.
Alisema miongoni mwa ajenda zinazojadiliwa ni pamoja na kuifanya AGN ilioanzishwa mwaka 1995 kuwa ni taasisi ya Afrika imara ya Afrika ambayo imeweza kuusimamia Mkataba wa Kyoto unaozitaka nchi wanachama kupunguza uzalishaji wa gesijoto.
Pia, Dkt. Muyungi alisema hatua nyingine ni kuwa na ukusanyaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi ulio wazi na kuhakikisha inakuwa chini ya Umoja wa Afrika na kuweka uelewa, kumbukumbu na historia ya mambo yanayofanyika.
Naye Mshauri Maalumu wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi Bi. Kholuthm Omar alisema mkutano huo ni muhimu kujadili namna bora ya kuwasaidia wakulima, wavuvi na wafugaji wanaoathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa Pili wa AGN ulioandaliwa chini ya uongozi wa Tanzania kwa ushirikiano na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) ni hatua kubwa ya kuunda mikakati ya Afrika ya mazungumzo ya hali ya hewa kwa mwaka 2025.