Tanzania yafaidika na miradi ya kupambana na hali ya jangwa

Jan, 25 2023

Katika kukabiliana na changamoto ya ukame, Tanzania imefaidika na miradi ya kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi hivyo kupunguza kuenea kwa hali ya jangwa na ukame na athari zake.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua kikao cha wataalamu cha kuhakiki rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa hali ya

Jangwa na Ukame (UNCCD) leo Januari 25, 2023 jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Mkuu, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Catherine Bamwenzaki amesema Mkoa wa Kilimanjaro unafaidika na mradi wa kuongoa maeneo yaliyoharibibika wakati Tabora na Katavi imefaidika na mradi wa kuhifadhi misitu ya miombo.

Bi. Bamwenzaki amebainisha kuwa Tanzania inafaidika pia na Mradi wa Kunusuru Vyanzo vya Maji Kupitia Usimamizi Endelevu wa Ardhi Katika Mabonde Madogo ya Ruvu na Zigi, Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula Katika Maeneo Kame ya Tanzania pamoja na Programu ya kuandaa Shabaha ya kuzuia uharibifu wa ardhi ifikapo mwaka 2030.

“Zipo faida kadhaa ambazo nchi wanachama wananufaika ambazo ni pamoja na kujengewa uwezo kitaalam, kifedha na kupatiwa vitendea kazi kwaajili ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame,” amesema.

Hivyo, kwa kuwa mwanachama wa Mkataba huu, Serikali pia kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imefanya tafiti mbalimbali na kuandaa taarifa ambazo zinatoa uelekeo utakaonesha njia ya kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji (UNCDF) Bi. Aine Mushi amesema Mkakati huo utakuja na ripoti ambayo itasaidia katika utekelezaji wake.

Aidha, amesema kuwa upo umuhimu wa kuona namna gani mkakati unashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo.

“Tunapowashirikisha wadau hawa tutaweza kujua ni kwa namna gani tunaingia kwenye mfumo wa bajeti ya Serikali na kwa kiwango gani cha fedha tunaweza kutekeleza mkakati huu,” ameongeza Bi. Aine.

Kikao hicho kimeshirikisha wawakilishi wa Wizara za kisekta wawakilishi wa washirika wa maendeleo, wawakilishi wa asasi za kiraia na wawakilishi wa sekta binafsi.

Settings