Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Sima: Serikali inaandaa mkakati kulinda uchimbaji endelevu


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amesema Serikali inaandaa mkakati wa muda mrefu unaotokana na mapendekeo ya Kamati Maalum ya wadau iliyoundwa na Ofisi hiyo kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kuwa na uchimbaji endelevu wa mchanga na usiokiuka Sheria za nchi.

Aliongeza kuwa zitafanyika tafiti na kuendeleza teknolojia za ujenzi zinazoweza kutumia mchanga kidogo na kuelimisha wananchi kuhusu athari za uchimbaji holela wa mchanga na kuzuia uchimbaji holela.

Aidha, Sima alisema kuwa mamlaka mbalimbali zikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mamlaka za Mabonde na Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Madini Mkoa wa Dar es Salaam, zimekuwa zikifanya ukaguzi wa mara kwa mara na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria huchukuliwa, “Kuhusu uchafuzi wa mazingira uliokithiri, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 Kifungu 139(1) imetoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuzuia au kupunguza taka ngumu, taka vimiminika, gesi taka na taka zenye madhara. Serikali itaendelea kuelimisha wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza Sima.