Sima awataka wauzaji mifuzo mbadala kutowakandamiza wananchi

Jun, 01 2019

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Sima amewataka wafanyabiashara wa mifuko mbadala kutotumia fursa hiyo kuwakandamiza wananchi kwa kuiuza kwa bei ya kubwa.

Mhe. Sima ametoa kauli hiyo leo mjini Singida wakati aliposhiriki operesheni ya kukagua utekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki ambalo limenza Juni mosi mwaka huu.

Katika opresheni hiyo iliyoambatana na ugawaji wa mifuko mbadala iliyotolewa na Kanisa la Full Gospel kwa wananchi mjini hapa alisema ni busara kwa wafanyabiashara hao kuweka bei inayowawezesha wananchi kuweza kuinunua.

“Ndugu wafanyabiashara tusiwakomoe Watanzania wasije kuona sasa mifuko hii ni ghali na kuona ni bora turudi katika mifuko ya plastiki ambayo imepigwa marufuku,” alisema.

Naibu Waziri Sima ambaye alikuwa mgeni rasmi katika operesheni hiyo

akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi alisema

wataalamu kutoka serikalini watatembelea viwandani kuona kama bei rafiki kwa mwananchi inatumika.

Aidha aliwataka wananchi hususan vikundi vya wanawake kutumia fursa hiyo kusuka vikapu kwa ajili ya kubebea bidhaa na hivyo kujipatia kipato ambapo alisema kwa kufanya hivyo tutajenga utamaduni kama wa zamani na kuachana na mifuko ya plastiki. Operesheni ya kukagua utekelesaji wa katazo la mifuko ya plastiki linaloratibiwa na Ofisi ya Makamu ilibaini wananchi wengi kupata uelewa wa madhara ya

mifuko ya plastiki.

Wananchi mbalimbali wameitikia wito wa kuanza kutumia mifuko mbadala katika masoko na maduka ambapo wamesema wanaipongeza Serikali kwa kuliona hilo na kupiga marufuku mifuko hiyo.

Zoezi hilo limeenda sambamba na utoaji wa elimu kuhusu madhara ya mifuko ya plastiki na fursa za uwekezaji wa mifuko mbadala kama ambavyo ilitolewa na wakaguzi kutoka Baraza la Taifa Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). Pia mkoa huo ulifanya maandamano ya kuunga mkono katazao hilo na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala ambapo yalihudhuriawa viongozi mbalimbali kutoka mkoa huo.

Settings