Serikali yawataka wataalamu na wadau wa mazingira kuibua miradi ya mazingira

Feb, 15 2023

Serikali imewataka wataalamu na wadau wa mazingira nchini kutumia vyema fursa za mafunzo yanayotolewa na wadau wa maendeleo ili kuibua ajenda na vipaumbele muhimu vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa Februari 14, 2023 na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga wakati wa hotuba yake ya kufunga Warsha ya siku mbili ya Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Mazingira wa Dunia (GEF).na kusomwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Dkt. Andrew Komba.

Bi. Maganga amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na GEF imeandaa warsha hiyo kwa ajili ya kuwakutanisha wataalamu na wadau wa mazingira ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya GEF mzunguko wa nane ambao unatarajia kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne ijayo.

“Warsha hii ilikuwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuanisha vipengele vya miradi ya GEF mzunguko wa nane na pia kupeana ujuzi na maarifa ya pamoja katika namna ya kukabiliana na athari za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi” amesema Bi. Maganga.

Akifafanua zaidi Bi. Maganga amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imekuwa ikiendesha mafunzo na warsha mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wataalamu na wadau wa mazingira wanaongeza ujuzi na maarifa katika usimamizi wa miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo.

Aidha Bi. Maganga amewahakikishia wadau wa maendeleo ikiwemo GEF kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kusimamia vyema miradi yote ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa malengo ya miradi yanafikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake Mratibu wa Mfuko wa GEF Kanda ya Afrika, Dkt. Ibrahima Sow amewashukuru wadau na wataalamu wa mazingira walioshiriki warsha hiyo kwa kuwasilisha na kutoa maoni na mapendekezo yatakayoisaidia utekelezaji wa miradi ya GEF- mzunguko wa nane.

Warsha hii imetusaidia kuona utayari wa wataalamu na wadau wa mazingira na Serikali kwa ujumla katika namna ya kuanza utekelezaji miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi awamu ya nane. Tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha malengo ya miradi hii inafikiwa” amesema Sow.

Maeneo matatu ya utekelezaji wa mradi wa GEF- mzunguko wa nane itajielekeza katika mradi wa usimamizi katika Maziwa Makuu na Mabonde ya Maji, fedha za kujenga uwezo kwa wataalamu wa miradi pamoja na usimamizi wa miradi katika nchi zinazoendelea.

Aidha Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalamu wa uhifadhi na usimamizi wa mazingira kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwemo maafisa wa Serikali, Taasisi, Idara na Wakala wa Serikali na Taasisi binafsi.

Wadau wengine ni Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mazingira Duniani (UNDP), Benki ya Dunia (WB), Shirika la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), IFAD na IUCN.

Settings