Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu baa na kumbi za starehe zilizokiuka utaratibu baada ya kubainika kupiga muziki uliozidi viwango katika mikoa mbalimbali nchini na hivyo kukiuka Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.
Imesema imeanza kuzifungulia baa na kumbi za starehe ambazo zimekidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 ambayo pamoja imeweka kiwango cha mitetemo ya sauti.
Ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni jijini Dodoma leo Mei 16, 2023 baada Mbunge wa Geita Vijijini Mhe. Joseph Musukuma kuomba mwongozo kupitia Kanuni ya 54(1) akisema taifa linakosa mapato kutokana na kufungwa kwa baa.
Waziri Jafo amesema hadi kufikia Mei 15, 2023 baa tano zilizofungiwa jijini Dodoma zimeshafunguliwa na tayari nne zimeshaanza kazi baada ya kukidhi matakwa ya Sheria hiyo.
Amesema hatua ya kufungia baa ilichukuliwa baada ya Serikali kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wannachi kuhusu uchafuzi wa mazingira kwa kelele katika maeneo hayo.
Hivyo, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2021 ilikutana na TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya, Wizara ya Sanaa na Utamaduni pamoja na Wizara ya Elimu na kuja na Mwongozo kuwabana wanasababisha changamoto hiyo.
Amefafanua kuwa pamoja na kutoa mwongozo huo kumekuwa na baadhi ya wamiliki wa maeneo ya starehe kutotii matakwa ya sheria na kusababisha athari kwa jamii ikiwemo watoto kupata changamoto ya usikivu na hata vifo.
Waziri Jafo amesema hivi karibuni Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka za Serikali za Mitaa ilifanya operesheni ya kukagua maeneo yanayolalamikiwa kwa kelele na kuwachukulia hatua.
Ameipongeza NEMC kwa kazi nzuri ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa njia ya kelele hatua iliyowafanya wamiliki wa maeneo ya starehe kufanya marekebisho kwa kudhibiti kelele.
“Maeneo ya kumbi za starehe yameainishwa kwa mfano night clubs (klabu za usiku) zenye sound proof (vizibiti sauti) na katika maeneo mengine ya baa kuna vifaa vya kupima sauti na ndio maana hivi karibuni taasisi yetu ya NEMC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa ilikuwa ikiwafuatilia wanaokiuka sheria na takriban baa 89 zilifungwa lakini asubuhi yake nikatoa maelekezo kwasababu wengi wao walishatii sheria na tumewaruhusu kufungua,” amefafanua.
Amesema kuwa wengi wa wamiliki wa baa wameanza kufunga vizuia sauti na hivyo kukidhi matakwa ya kisheria hata iliyoifanya Serikali kuwaruhusu kufungua na kuendelea kutoa huduma.