Serikali yatambulisha mradi mpya wa kimazingira

Sep, 29 2022

Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaongezewa uwezo wa kutambua na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao.

Amesema hayo wakati wa kikao cha Kikao cha Kutambulusha na Kuandaa Mradi wa Kujenga Uwezo wa Utayari wa Nchi Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi kilichofanyika leo Septemba 29, 2022 jijini Dodoma.

Dkt. Komba alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha mipango ya masuala ya kuhimili madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanaingizwa katika mipango ya Serikali katika ngazi zote.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi utasaidia katika kutoa tathmini ya kina ya kitaifa yenye msingi wa kubuni mbinu za kukabiliana na athari hizo zinazoikabili nchi na dunia kwa ujumla.

“Baada ya kikao hiki cha leo ambacho kimekutanisha wadau mbalimbali tunatarajia sasa halmashauri, kata na vijiji vitawezeshwa kutambua na kuweka afua za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.

“Mabadiliko ya tabianchi yanaleta hatari kubwa ya kimazingira, kijamii na kiuchumi na hivyo kuna haja ya mwitikio wa haraka wa kitaifa na kimataifa katika kukabiliana na athari zake,” alisema Dkt. Komba.

Aliongeza kuwa Tanzania inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na joto kali, kupanda kwa kina cha bahari na kuongezeka kwa mvua na athari hizo zimesababisha mafuriko ya mara kwa mara yanayoathiri nyanja za kijamii na kiuchumi hasa miundombinu, makazi ya watu, uharibifu wa mifumo ikolojia.

Athari zingine ni ukame wa mara kwa mara, kuyeyuka kwa barafu ya milimani, kuenea kwa wadudu na magonjwa ya mazao, mabadiliko ya maeneo ya kilimo-ikolojia na kupungua kwa mavuno ya mazao, asidi ya bahari, kuingilia maji ya bahari kwenye rasilimali za maji safi na mabadiliko ya matumizi ya ardhi.

“Ndugu za ngu athari hizi zote za mabadiliko ya tabianchi zinatishia usalama na maisha ya wananchi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla,” alitahadharisha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambao ndio wafadhili wa mradi huo, Bw. Amon Manyama alipongeza Serikali kwa maandalizi ya mradi huo.

Bw. Manyama alisema UNDP inatambua utayari na mchango wa Serikali, wadau na taasisi zisizo za kiserikali katika utekelezaji wa mradi huo ambao ulipitishwa Agosti 2022 na kutatajiwa kukamilika mwaka 2024.

Mradi huo unatekelelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Ofisi ya Makamu wa Kwanza kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Settings