​Serikali yaandaa Mkakati wa kuhigfadhi mazingira Ukanda wa Pwani

Nov, 08 2021

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa.

Chande amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Mhe. Amour Khamis Mbarouk aliyetaka kufahamu je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha makundi ya wananchi ili kuhamasisha uhifadhi wa mazingira hasa katika Fukwe za Bahari ya Hindi.

Alisema kutokana na utekelezaji wa Mkakati huu, na kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeanzisha Vikundi vya Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi vinavyofahamika kama “Beach Management Units – BMUs.

Naibu waziri alifafanua kuwa vikundi vilivyoanzishwa katika ngazi ya Kijiji/Mtaa kwa mujibu wa Kifungu cha 18 cha Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003. Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi una jumla ya vikundi 157 ambapo Tanga (31), Pwani (46), Dar es Salaam (23), Lindi (46) na Mtwara (11).

Aidha, akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo alisema Serikali ina mpango wa kuwashirikisha viongozi wa dini na Taasisi zao katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uhifadhi wa mazingira.

Settings