Serikali kutumia Dola Bilioni 19 kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Oct, 03 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo takribani Dola bilioni 19.2 za Marekani zitatumika katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko Tabianchi.

Amesema hayo juzi katika kikao cha Wadau wa Mazingira kinachofanyika jijini Arusha kwa muda wa siku nne kujadili mikakati ya nchi kuongeza uwezo wa kupata fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Waziri Jafo alisema Serikali inachukua hatua kubwa kama vile kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

“Tanzania pia imetekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kuta katika fukwe mkoani Mtwara na Visiwani Zanzibar pamoja na miradi mingine katika sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, misitu, viwanda, TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi,” alisisitiza Dkt. Jafo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Dadi Shajak alisema kwa upande wa Zanzibar kikao kazi hiki pia kitaweka mikakati ya kupata fedha zitakazotumika pande zote mbili za Muungano.

Alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri upande wa Zanzibar kwa kusababisha kupanda kwa kina cha maji ya bahari na mmomonyoko wa udongo maeneo ya pwani.

“Kama tunavyojua utalii mkubwa wa Zanzibar upo katika maeneo ya baharini hivyo fukwe zinaharibika kutokana na athari za mabadiliko ya tabia na ndio maana tunapambana kujenga kuta na kupanda mikoko ili kuzuia,” alisema.

Pia Katibu Mkuu huyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika bajeti yake imetenga Sh. Bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa kuta na Sh. Bilioni 1.1 kwa ajili ya upandaji mikoko.

Nae Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba amesema kwa muda wa siku nne mashirika ya kitaifa, asasi za kiraia na taasisi za kifedha pamoja na mambo mengine watapitia msimamo wa Tanzania kuelekea Mkutano wa 27 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi utakaofanyika Novemba 6 hadi 8, 2022, Sharma el-Sheikh, Misri.

“Sisi sote ni mashahidi tuna matatzio makubwa nchini jua linawaka sana, joto kali, mvua hazinyeshi hizi ni athari za mabadiliko ya tabianchi hivyo tunaendelea na jitihada za kupambana na changamoto hizi,” alisema Dkt. Komba.


Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kila nchi inatakiwa kuonesha mkakati wa namna ya kupambana na mabadiliko tabianchi kwa kupunguza uzalishaji wa gesi joto.


Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na ni miongoni mwa nchi zilizowasilisha mchango wake wa Kukabiliana na athari hizo kwenye Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Julai 30, 2021.

Settings