Serikali imesema kamwe haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji wanaolenga kuwekeza katika sekta ya viwanda bali maendeleo ya viwanda ni lazima yaende sambamba na hifadhi ya Mazingira.
Rai hii imetolewa leo Februari 24, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo katika ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira katika Kiwanda cha A One product and Bottles Ltd katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Dkt. Jafo amesema Serikali inahimiza wawekezaji nchini lakini ni vema wawekezaji hao wazingatie Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa ukamilifu wake. Katika ziara ya kukagua kiwanda hicho kinachozalisha vinywaji baridi (soda, maji na juisi).
Waziri Jafo amepongeza utii wa Kiwanda hicho kwa kutekeleza kwa wakati maagizo ya Serikali ya kutotumia karatasi za plastiki kwenye vifuniko vya chupa za maji.
“Kiwanda hiki kimenifurahisha sana, wametii kwa vitendo maagizo ya Serikali ya kutotumia karatasi za plastiki kwenye vifuniko vya chupa za maji yanavyozalishwa na Kiwanda hiki. Kiwanda hiki pia kimeanzisha kiwanda cha kurejeleza chupa za plastiki, hata zile za rangi ambazo ukusanyaji wake umekuwa na changamoto, natoa rai kwao kuhakikisha chupa zao hazisambai katika mazingira bali wanazirejesha kiwandani na kutengeneza bidhaa nyingine” Dkt. Jafo alisisitiza
Amesema, viwanda vina mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi sambamba na kuchangia ajira za moja kwa moja hivyo Serikali itahakikisha matakwa ya Sheria yanazingatiwa.