Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema kuwa hadi sasa hakuna changamoto mpya za Muungano zilizojitokeza.
Amesema hayo leo Mei 17, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Angelina Adam Malembeka aliyetaka kufahamu changamoto gani mpya za Muungano zimejitokeza.
Wakati huo akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohamed Haji aliyeuliza kwanini Halmashauri ya Magharibi ‘A’ imeweka Sheria ya Kodi na VAT kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, Mhe. Khamis amesema Serikali ya SMT itashirikiana na serikali ya SMZ kufuatilia utaratibu unaotumika.
Amesema Fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Sura 96 ya mwaka 2009 na zinatumika kwa kuzingatia Miongozo, Kanuni na Taratibu za usimamizi wa fedha za umma.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa kila upande wa Serikali zote mbili una utaratibu wa usimamizi wa matumizi ya fedha za uma huku akisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa pande zote mbili kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii na kuwaletea wananchi maendeleo.