Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

Rais Samia aihimiza Jamii kupanda miti Kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameihimiza jamii kupanda miti ya kutosha lengo likiwa ni kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ambayo yameanza kuleta athari katika mazingira.

Mhe. Samia amesema hayo leo Novemba 23, 2022 katika Mkutano wa Hadhara na Wananchi wa Babati mkoani Manyara uliofanyika katika Uwanja wa Kwaraa, ambapo amesema jamii inapaswa kuacha kukata miti na badala yake wapande miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali.

“Tumekata miti vya kutosha sasa twendeni tukapande miti, lakini ile ambayo bado ipo tuache kuikata ili mazingira yarudi, maji yapatikane, umeme upatikane na mazingira yawe bora zaidi,” alisema.

Hivyo, kutokana na hali hiyo Mhe. Rais Samia alitoa wito kwa wanamazingira wa mikoa na wilaya kote nchini kuanza kushughulikia changamoto hizo za kimazingira.

Aidha Mhe. Rais Samia alisema kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinajitokeza kwenye maziwa ambapo hivi sasa tunashuhudia maziwa yakikauka na wakati mwingine yanajaa kwa kasi na kuingia kwenye mkazi ya watu.

Aliwataka wananchi kuacha kuharibu mazingira kwani kitendo hicho kinasababisha mabadiliko ya tabianchi ambayo huchangia joto kuwa kali na mvua kukosekana na hivyo mifugo hufa kwa kukosa malisho na maji.

"Nawaasa kupunguza migogoro baina yenu hasa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inaharibu taswira ya nchi yetu, nawasihi pia wanasiasa kuacha tabia ya kuchochea migogoro hiyo bali kuwa mstari wa mbele kusimamia mipango bora ya matumizi bora ya ardhi", amesema Mhe. Samia.