Habari
Ofisi ya Makamu wa Rais, wadau wa mazingira kushirikiana
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha ushirikiano kitaifa na Kimataifa hasa katika masuala ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.
Dkt. Muyungi amesema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuwa kiungo katika mashirikiano na wadau ambao wanaonesha nia njema katika nyanja hiyo sambamba na masuala yanayohusu Uchumi wa Buluu.
Amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) Bi. Lorence Ansermet aliyeambatana na Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) nchini Tanzania Bi. Clara Makenya.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi za Makamu wa Rais, Mtumba, Dodoma Mei 6,2026 ambapo Dkt. Muyungi amesema suala la mazingira linahusu kila jamii hivyo kila mtu anapaswa kuwa mlinzi na balozi wa eneo linalomzunguka.
Dkt. Muyungi amewashukuru kwa ujio wao ambao umesaidia kujadili mambo mbalimbali ya ushirikiano kuhusu namna ya kuisaidia na kuongeza ushirikiano katika kuendeleza miradi inayohusu mazingira.



