Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kutoa elimu ya Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu ili kuhakikisha Watanzania wanafahamu vyema majukumu ya ofisi hiyo kupitia fursa mbalimbali zilizopo.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe wakati alipotembelea Banda la Ofisi hiyo katika Maonesho ya 32 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni Jijini Dodoma. leo Jumamosi (Agosti 2, 2025).
Prof. Msoffe amesema Serikali inatambua hamasa waliyonayo Watanzania katika kujifunza masuala ya Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu, hivyo kwa kutambua umuhimu huo Ofisi hiyo imekuwa ikishiriki katika maonesho hayo ili kuelimisha jamii na Watanzania kwa ujumla kuhusu fursa zilizopo kupitia mazingira na uchumi wa buluu.
“Katika maonesho haya, Ofisi imekuja na masuala mahsusi ya kuelimisha wananchi kuhusu Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu...wadau na wananchi watajifunza kuhusu biashara ya kaboni, umuhimu wa kutunza, kuhifadhi mazingira na namna ya kugeuza taka kuwa fursa” amesema Prof. Msoffe.
Amefafanua kuwa kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa nyaraka mbalimbali ikiwemo sera, sheria, mikakati na mipango mbalimbali ambapo wananchi wataweza kujionea juhudi na hatua stahiki zilizochukuliwa na Serikali katika kuhifadhi na kutunza mazingira.
Kwa mujibu wa Prof. Msoffe, katika kuongeza wigo wa elimu ya mazingira, Taasisi za Ofisi hiyo ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pia inashiriki maonesho hayo ikiwa ni njia mahsusi ya kuelimisha jamii na Watanzania kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira.
Prof. Msoffe amesema katika maonesho hayo pia, Ofisi ya Makamu wa Rais imepanga kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu uchumi wa buluu na fursa zinazoweza kuibuliwa kupitia rasilimali na mazao mbalimbali yanayopatikana katika mito, bahari na maziwa.
Ameeleza kuwa eneo lingine litakalopewa msukumo wa elimu kwa wananchi na wadau ni kuhusu biashara ya kaboni ambayo imeendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali duniani na hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais imehakikisha Watanzania pia wanabaini fursa za biashara hiyo ili kujiinua kiuchumi.
Kuhusu elimu ya Muungano, Prof. Msoffe amesema wananchi na wadau watakaotembelea Banda la Ofisi hiyo pia watapata uelewa kuhusu Muungano ikiwemo historia na chimbuko la Muungano na mafanikio yake yaliyofikiwa hadi sasa.