Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kushirikiana kuandaa mwongozo utakaosaidia katika udhibiti wa taka za kielektroniki kuokoa ikolojia ya mazingira na afya za binamu.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi wakati wa Warsha ya Kuandaa Mwongozo ya Kudhibiti Taka za Kielektroniki na Umeme iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema warsha hiyo itasaidia washiriki kutafakari kuhusu changamoto za taka za kielektroniki ambazo nyingi zinatoka nje ya nchi zinakuja kama vifaa vilivyotumika kwa ajili ya kutumika tena na baadaye kutupwa na kuwa taka hatarishi zinazosababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.
“Tafiti nyingi zinaonesha kuwa miongoni mwa vifaa vya kielektroniki na umeme vilivyotumika vimeonekana asilimia kubwa havifanyi kazi na matokeo yake vinasambaa katika maeneo yetu tunayoishia na kuleta madhara,” alisema Mitawi.
Aliongeza kuwa baadhi ya vifaa vya aina hivyo vina mchanganyiko wa kemikali tofauti ambazo zihusika katika utengenezwaji wa vifaa kamili kwa ajili ya matumizi na zimetangazwa kimataifa kuwa ni sumu hivyo hazipaswi kuwepo tena sokoni.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo alisema baadhi ya nchi wanachama wa EAC zimeona ipo haja na umuhimu wa kuwa na warsha ya pamoja inayohusisha taasisi zake katika jumuiya hiyo kujadili na kuwa na uelewa wa pamoja katika kusimamia na kudhibiti uingizaji wa vifaa vyote vya kielektroniki na umeme vilivyotumika vinavyoingia katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na hivyo kuja na mikakati ya pamoja ya kuweza kushughuliki changamoto hiyo.
“Tumeelezwa hapa na wawakilishi kutoka Ujerumani kuwa makontena zaidi ya milioni tisa huingia na vitu vilivyotumika kwa hiyo bila kuwa na jitihada za pamoja sasa katika jumuiya yetu itakuwa ngumu kudhibiti uingizaji wa vifaa hivyo ambavyo vimekwisha tumika na havifanyi kazi na kuingizwa kama taka katika nchi wanachama wa jumuiya za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania” alisisitiza Mitawi