Naibu Waziri Khamis: Serikali imetenga milioni 661/- kujenga fukwe Zanzibar

May, 14 2024

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imetenga shilingi milioni 661 kutekeleza miradi ya ujenzi wa fukwe Zanzibar.

Amesema hayo bungeni leo tarehe 14 Mei, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Mhe. Suleiman Haroub Suleiman aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kutengeneza fukwe za bahari zilizoathirika upande wa Zanzibar.

Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Khamis amesema kuwa kati ya fedha hizo zilizotengwa kiasi cha shilingi milioni 300 zitatumika kukamilisha ujenzi wa matuta ya kuzuia maji ya bahari kuingia sehemu ya mashamba ya mpunga katika Shehiya ya Kwa Mgogo Kusini Pemba katika Ufukwe wa Sipwese.

Pia, amesema shilingi milioni 361 zitatumika kwa ajili ya kufanya tathmini katika eneo la Nungwi Visiwani Zanzibar ili kusanifu namna bora ya kuthibiti uharibifu unaoendelea.

Akijibu swali la nyongeza kuhusu mkakati wa Serikali wa kurekebisha fukwe kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Naibu Waziri Khamis amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar (SMZ) inatekeleza ya kimazingira.

Amebainisha kuwa miradi ya ujenzi wa kuta inatekelezwa katika maeneo ya fukwe ambayo inasaidia maji ya bahari yasiingie nchi kavu na kuleta madhara kwa wananchi na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande mwingine Mhe. Khamis ameliarifu Bunge kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa matuta ya kuzuia maji ya bahari katika eneo la Mtambwe Mkuu Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Naibu Waziri Khamis amesema hayo alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyeuliza kuhusu ni lini Serikali itajenga matuta kunusuru makazi ya watu kwa maji ya bahari.

“Ni kweli Mheshimiwa Naibu Spika ni kweli tunatambua kwamba kuna hiyo changamoto huko Mtambwe lakini nimuombe tu mheshimiwa (mbunge) tunamaliza ukuta wa Sipwese Kusini Pemba, tukimaliza tunakuja Mtambwe, Kaskazini Pemba,“ amefafanua Naibu Waziri.

Katika hatua nyingine kuhusu suala la usafi wa fukwe za Zanzibar amesema SMZ kupitia halmashauri, manispaa, mabaraza ya miji na majiji yameanza kuchukua hatua ya kusimamia usafi wa kila mwezi kupitia Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) Msingiri inaendelea na zoezi la kusafisha maeneo mbalimbali.

Settings