Naibu Waziri Khamis azitaka halmashauri kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji fedha za miradi

Feb, 24 2023

Serikali imeziagiza halmashauri za wilaya zote nchini zinazotekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa fedha zinatolewa na Serikali, Wadau na wafadhili ili kuwezesha miradi hiyo kuleta tija kwa wananchi.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya LDFS inayofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na kuratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza

Amesema Serikali imeendelea na juhudi za kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kutoka kwa wadau na wafadhili mbalimbali ikiwa ni juhudi za kuibua na kuendelea miradi ya maendeleo kwa wananchi.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya ziara katika mataifa mbalimbali kwa ajili ya kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha ili kutekeleza miradi. Nawasihi Viongozi na Watendaji tuliopewa dhamana ya miradi hii, tuhakikishe tunasimamia vyema fedha hizi zinazoelekezwa katika miradi ili kuleta matokeo chanya” amesema Mhe. Khamis.

Aidha, naibu waziri huyo amesema dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ni kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa kupitia program ya LDFS inaleta manufaa kwa wananchi ikiwemo Kuboresha mifumo ikolojia ya kilimo ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kuboresha mazingira katika Halmashauri za wilaya husika.

Akifafanua zaidi amesema manufaa mengine ya miradi hiyo ni pamoja na kuboresha usimamizi endelevu wa mifumo ikolojia inayochangia kutoa huduma muhimu za uzalishaji kwenye maeneo ya ardhi, maji, misitu, bioanuai kwa madhumuni ya kuboresha uzalishaji.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa LDFS Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Ngusa Buyamba amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Februari 2018 ukiwa na thamani ya sh.milioni 813 ambapo hadi sasa halmashauri hiyo imepokea sh.miliioni 403 kutoka serikalini.

Buyamba ameitaja miradi inayotekelezwa ni visima vya maji, ufugaji wa kuku na kondoo, ufugaji nyuki, shamba darasa ambayo inatakelezwa katika vijiji vya Nyang’hanga, Iseni, Lemeji na Ng’haya vilivyopo katika Kata za Sukuma na Ng’haya.

“Tunaishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kutupatia fedha kwa wakati kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii ambayo ina faida kubwa ikiwemo kuimarisha mifumo ya matumizi ya ardhi na upatikanaji wa hifadhi ya rasilimali. Tunaahidi kutumia vyema fedha hizi katika malengo yaliyokusudiwa” amesema Buyamba.

Naye Diwani wa Kata ya Sukuma Faustine Makingi aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu Rais kwa kuendelelea kusimamia kwa karibu miradi hiyo na kuongeza kuwa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo litahakisha maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Naibu Waziri yanazingatiwa na kutekelezwa.

Mhe. Naibu Waziri Khamis yupo katika ziara ya kikazi katika Mikoa wa Mwanza na Tabora kwa ajili ya kutembelea miradi mbalimbali ya mazingira inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Settings