Naibu Waziri Khamis atoa maagizo mazito kwa Kamati za Ulinzi na Usalama, NEMC

Feb, 22 2023

Serikali imezitaka kamati za ulinzi na usalama katika Mikoa na Wilaya zote nchini pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuanzisha operesheni ya kuwaibaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria waagizaji na wasambazaji wa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku na Serikali.

Agizo hilo limetolewa leo Februari 22, 2023) Jijini Mwanza na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi wa dampo la kisasa lililojengwa Kata ya Buhongwa Jijini Mwanza.

Naibu Waziri Khamis amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kutokana na athari za mazingira na pia mifuko hiyo kuwa hatarishi kwa afya za wananchi, hata hivyo wapo baadhi ya watu wamekuwa wakikiuka katazo la matumizi ya mifuko hilo lililotolewa na Serikali mwaka 2019.

“Tumeona katika dampo hili la Buhongwa limekuwa ni kituo cha mifuko ya plastiki, hii imeonesha kuwa huko mitaani kuna watu wanaojishughulisha na biashara ya uagizaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki isiyo na ubora. Naziagiza Kamati za Ulinzi, NEMC na Mabaraza ya Halmashauri ya Wilaya kusimamia mianya yote inayopenyeza mifuko hii” amesema Naibu Waziri Khamis.

Aidha Naibu Waziri Khamis amesema nadharia za kisayansi zimedhibitisha kuwa mifuko ya plastiki inaathari kubwa kimazingira kutokana na kuchukua kipindi kirefu kutekeleza na kuoza kuanzia miaka mitatu na kuendelea na hivyo kuleta tishio kwa kubwa kwa maisha na ustawi wa viumbe na binadamu.

Akifafanua zaidi Naibu Waziri Khamis amesema Serikali ya Awamu ya Sita kamwe haitorudi nyuma katika katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki na kuwataka watu wachache wanaojishughulisha na biashara ya uagizaji na usambazaji wa biashara hiyo kuacha mara moja kabla ya kukamatwa na kufikishwa katika na mkono wa sheria.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuanzisha mradi huo ambao utasaidia juhudi za Serikali za kutotumia fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa tiba kwa kuwa taka zinazozalishwa katika Jiji la Mwanza zitapelekwa kwa wakati katika dampo hilo na kunusuru magonjwa ya mlipuko.

Akifafanua zaidi Naibu Waziri Khamis amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa mapambano ya uharibifu wa mazingira na katika kudhibitisha kauli kwa vitendo ametoa kiasi cha TZS Bilioni 3 kwa kila Halmashauri nchini kwa ajili ya kuanzia miradi ya ujenzi madampo ya kisasa ynayochakata taka kisayansi na kulinda afya za wananchi.

Akizungumzia ujenzi wa mradi wa dampo hilo, Meneja mradi wa dampo hilo kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Desderius Polle amesema ujenzi wa dampo lenye ukubwa wa hekta 34 uliokamilika mwaka 2020 una thamani ya kiasi cha TZS Bilioni 8.9 na unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Programu ya Uendelezaji wa Majiji ya Kimkakati Tanzania (TSCP).

Polle amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa shimo la kuhifadhi taka ngumu lenye ukubwa wa mita za mraba 39,000, ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa Kilomita 0.7, ujenzi wa barabara ya changalawe yenye urefu wa kilomita 1.8, ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji ya mvua, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua, upandaji wa miti na uwekaji wa taa za barabarani na maegesho ya mitambo na uchimbaji visima.

Naye Diwani wa Kata hiyo ya Nyamagana, Joseph Kabadi ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi wa dampo hilo la kisasa ambalo litakuwa suluhisho wa utunzaji wa mazingira kwa kuwa taka ngumu zitakuwa zikiteketezwa kwa wakati na hivyo kulinda za afya za wananchi wanaozunguka Kata hiyo.

Naibu Waziri Khamis yupo katika ziara ya kikazi Jijini Mwanza yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazohusu sekta ya mazingira nchini.

Settings