Naibu Waziri Khamis aridhishwa maendeleo ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais

Sep, 16 2022

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Septemba 16, 2022.

Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo Mhe. Khamis alionesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo akimtaka mkandarasi Kampuni ya SUMA JKT kuongeza kasi ya ujenzi ili likamilike na hatimaye lianze kutumika.

Ameitaka Kampuni ya SUMA JKT ambayo imepewa kazi ya kutekeleza mradi huo kuzingatia viwango vya ubora na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

"Pamoja na kuwa mradi huu tunatakiwa tuukamilishe mwakani natoka rai kwenu kazi hii ifanyike usiku na mchana, ili ikamilime mapema zaidi" Alisisitiza Naibu Waziri.

Akitoa maelezo ya awali Mhandisi Sajid Lukizo kutoka SUMA JKT amesema mkandarasi ameshakamilisha kazi ya ujenzi wa mradi kwa asilimia 38 na kuwa wana matumaini ya utakamilika kwa wakati.

Ofisi ya Makamu wa Rais ilisaini mkataba wa sh. bilioni 18.8 na Kampuni ya SUMA JKT wa kuanza ujenzi huo Oktoba 13, 2021 na unatarajia kukamilika mwezi Novemba, 2023.

Settings