Naibu Waziri Khamis ahimiza wadau kuendelea kutoa elimu ya mazingira

May, 26 2023

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Khamis Hamza Khamis amevitaka vyombo vya habari, taasisi na wadau wa mazingira kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza leo Mei 26, 2023 wakati wa hafla ya zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Buigiri iliyopo Kata ya Buigiri Wilaya ya Chamwino jijini Dodoma, Naibu Waziri Khamis amesema suala la uhifadhi wa mazingira ni jambo mtambuka linalohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.

Mhe. Khamis amesema viongozi wakuu wa dunia kila wakutanapo katika vikao na mikutano mbalimbali hujadili kwa kina masuala muhimu ya kidunia ikiwemo ajenda ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira ambapo umuhimu wake unabeba mustakabali wa viumbe hai, rasilimali na maliasili zilizopo katika uso wa dunia.

“Mabadiliko ya tabianchi ni ongezeko la muda mrefu la joto la wastani la dunia na kusababisha kubadilika kwa mfumo mzima wa hali ya hewa, ili kuinusuru jamii yetu kutoka kwenye changamoto hizi tunapaswa kupanda miti kwa wingi ili kuokoa maisha ya viumbe hai wengine pamoja na binadamu” amesema Naibu Waziri Khamis.

Aidha amesema kuwa upandaji miti na uhifadhi wa misitu ni moja ya hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo kwa kutambua umuhimu huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza Kampeni ya kupanda miti mashuleni ijulikanayo "SOMA NA MTI" yenye lengo la kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Naibu Waziri Khamis amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwafanya wanafunzi waone zoezi la upandaji miti kuwa ni sehemu ya maisha yao ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame na uhaba wa maji.

Ameongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi nchini katika kuhakikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira inakuwa na mafanikio ikiwemo kuwawezesha vijana kupata elimu sahihi ya utunzaji wa miti na kuchangia uhifadhi wa mazingira kwa weledi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Tabora Carbon Credit Harvest (TCCHP) iliyodhamini hafla hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Habari Conservation Organisation, Bernard Mwanawille amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira ikiwemo uhamasishaji wa jamii katika zoezi upandaji wa miti.

“Pamoja na kuhamasisha jamii uhifadhi na utunzaji wa mazingira, mwaka 2019 Shirika letu limeingia mkataba na Serikali katika uzalishaji wa biashara ya kaboni katika Mkoa wa Tabora ambayo tayari tumepatiwa misitu ya serikali ya mkoa na Wilaya” amesema Mwanawille.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya HCO ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Wilaya ya Chamwino (CCM) Mhe. Riziki Lulida amesema ajenda ya Dodoma ya kijani na Tanzania ya kijani inawezekana iwapo kutakuwepo ushirikiano wa pamoja baina ya serikali, jamii na wadau katika suala la uhamasishaji wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Mwaka 1973, Hayati Baba wa Taifa alifika Wilaya ya Chamwino na kuweka wazo la kuanzishwa kwa makazi ya Serikali katika Jiji la Dodoma huku akihimiza suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kuanzisha misitu ya asili. Tutahakikisha wazo lile tutaendelea kulienzi hususani kwa wakati huu kwa kuhimiza jamii yetu kupanda miti kwa wingi” amesema Mhe. Lulida.

Aidha, Mwakilishi wa Taasisi ya Habari Conservation Orgnanisation, Lazaro Balangu amesema mazingira ni nyumba ya wote hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kutunza, kuhifadhi na kuendeleza kwa kuwa ni rahisi sana kuharibu mazingira na ni vigumu sana kuyatengeneza.

“Shirika linapendekeza kila kijiji, kata iwe na bustani ama shamba la miti lisilopungua heka mbili. Kila Kaya ipande miti kulingana na idadi ya watu waliomo katika kaya husika na wale wanaotarajia kuzaliwa kwani wapo wanaodhani kuwa jukumu la kuhifadhi mazingira ni la serikali au taasisi au vikundi fulani” amesema Balangu.

Zoezi hilo la upandaji miti liliongozwa na Viongozi wa Chama na Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambapo jumla ya miche miti ya matunda na vivuli 1070 ilipandwa katika Shule ya Sekondari ya Buigiri.

Settings