Naibu Waziri Chande atoa rai kwa taasisi za elimu kuanzisha vitalu vya miche

Nov, 21 2021

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamad Hassan Chande mwishoni mwa wiki ameshiriki katika zoezi la upandaji miti lililoandaliwa na Taasisi ya Bright African Environment Development Group na kusisitiza kuwa ni kitendo cha kuigwa na kupongezwa na hivyo kutoa rai kwa jamii kuiga mfano huo.

Mhe. Chande ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo inayomiliki Shule ya Bright African kwa kusimamia mazingira kwa vitendo hasa uanzishaji wa vitalu vya miche ya miti na matunda kwa wanafunzi wake.

Amesema sasa hivi jamii inakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa Mazingira ambao umechangia matatizo mengi yanayoathiri maendeleo ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na upungufu wa umeme na mgao wa maji.

“Mmefanya jambo jema sana kuanza kuwapa ujuzi wanafunzi juu wajibu na umuhimu wa kutunza Mazingira. Hii ni jitihada inayopaswa kuungwa mkono na kujenga kizazi ambacho kinajua faida za kutunza Mazingira na kuepusha uharibifu wake” Chande alisisitiza.


Pia ameitaka Shule ya Bright African kushiriki katika programu mbalimbali za mazingira zinazoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ikiwa ni pamoja shindano linalohusisha Kampeni Kabambe ya Kitaifa ya Uhifadhi na Usafi wa Mazingira inayondeshwa na Ofisi yake ili kujifunza uhifadhi wa Mazingira.

“Serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kuhifadhi Mazingira ili kuifanya nchi yetu iwe na mazingira mazuri yanayoweza kutupatia maendeleo endelevu” Alisisitiza Naibu Waziri Chande.

Taasisi ya Bright African Environment Development Group iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam imejikita katika kuwapa maarifa wanafunzi kwa vitendo katika uhifadhi wa mazingira kwa mujibu wa mitaala ya elimu. Shule hiyo ina miche ya mititakriban 3000 ambayo itapandwa katika eneo la shule na kila mwanafunzi atapaswa kuwa na miti miwili ya kutunza hadi atakapo hitimu shule.




Settings