Mradi mpya SUSTAIN Eco kuwa mwarobaini wa upotevu wa misitu

May, 24 2023

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Bw. Abdallah Hassan amesema kumekuwa na upotevu wa hekta 490 za misitu kila mwaka hivyo kusababisha hali ya jangwa, upungufu wa maji na chakula.

Amesema hayo Mei 23, 2023 jijini Mbeya wakati akizindua Mradi wa SUSTAIN Eco unaosimamiwa na Taasisi ya International Union for Conservation of Nature (IUCN) wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 4.5 sawa na shilingi bilioni 11.

Mradi huo utahusika na usimamizi shirikishi wa ikolojia katika masuala ya Serikali, biashara na jamii husika, ili kuleta uwiano katika vipaumbele na ukuaji endelevu.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Mitawi alisema Tanzania imekuwa ikiathiriwa na kutokuwepo kwa usawa wa bionuai na hivyo kusababisha kutokea kwa migogoro kati ya makundi mbalimbali hususan ya wakulima na wafugaji.

Hivyo, kutokana na hali hiyo amewataka wadau wengine kujihusisha na masuala ya mazingira akibainisha kuwa uhai wa binadamu na viumbe vingine vyote unategemea mazingira.

Ametoa shukrani kwa Serikali ya Sweden pamoja na Taadidi ya IUCN kwa kuonesha ushirikiano katika kuyajali mazingira jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa nchi yetu.

Kwa upande wake Mkuu wa IUCN Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika Bw. Charles Oluchina ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuonesha ushirikiano mzuri katika usimamizi wa mazingira.

Pia, ameishukuru Serikali ya Sweden kwa kufadhili masuala ya mazingira na hasa Mradi wa SUSTAIN Eco akisema kuwa fedha hizo zitasaidia katika kubadilisha, kuhabarisha, kuimarisha matumizi ya rasilimali na kuzifanya ziwe endelevu.

“Usimamizi wa mazingira, bioanuai na mabadiliko ya tabianchi ni suala endelevu na kwa kuwa tarehe 22 mwezi Mei,2023 ilikuwa Siku ya Bionuai Duniani, hivyo uzinduzi wa mradi huu umefanyika kwa wakati muafaka,” alisema Bw. Olunuchi.

Nae, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Bi. Charlotte Ozaki Macias alisema kuwa mwaka 2023, Serikali ya Sweden inaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano pamoja na Serikali ya Tanzania na kwamba 22/5/2023 ilikuwa siku ya maadhimisho ya bionuai bado kuna ongezeko la jangwa, upungufu wa maji, wanyama na viumbe vingine vinazidi kupungua.

Aliongeza kuwa ongezeko la watu duniani nalo, limechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi akisisitiza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kuwe endelevu.

Mwakilishi wa Taasisi ya IUCN Tanzania ambaye pia Meneja wa Programu ya SUSTAIN ECo, Bw. Anthony Mhagama alieleza kuwa mradi huo ambao unasimamiwa na IUCN, utafanya kazi kwa kushirikiana na African Wildlife Foundation (AWF) pamoja na SNV katika katika maeneo matatu ambayo ni Kilombero, Katavi na Morogoro.

Settings