Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ahimiza usimamizi wa mazingira

Jun, 04 2023

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabiri Shekimweri amewataka viongozi na watendaji wa mitaa na kata kushirikiana na maafisa usafi na mazingira wa Halmashauri za Miji na Majiji katika kusimamia zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo yao.

Ametoa rai hiyo leo Jumapili (Juni 4, 2023) mara baada ya kukamilisha zoezi la usafi wa mazingira katika eneo la Ilazo Manispaa ya Dodoma ambapo aliambatana na watendaji mbalimbali wa Serikali, wananchi na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Mkoa wa Dodoma ikiwa ni shamrashamra za kuelekea wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.

Shekimweri amesema asilimia kubwa ya maradhi yote yanayotokea duniani kisayansi yanatokana na matokeo ya uchafu na hivyo amewataka watendaji wa mitaa na kata kuhakikisha zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya makazi ya wananchi na biashara yanapewa kipaumbele ili kutunza na kuhifadhi mazingira

“Tumefanya usafi katika mitaro, barabara, makazi ya watu na maeneo ya biashara katika eneo hili la Ilazo na kubaini kuwa kuna wingi wa taka ikiwemo mifuko ya plastiki, chupa za maji na maji taka hii ni wazi kuwa suala la usafi wa mazingira halijapewa msukumo na viongozi, watendaji na wananchi” amesema Shekimweri.

Kwa mujibu wa Shekimweri amesema ni wajibu maafisa usafi na mazingira wa Halmashauri za Miji na Majiji kuhakikisha kuwa wanazisimamia vyema kampuni na vikundi vya usafi wa mazingira ambavyo vimeajiriwa kwa ajili ya kufanya usafi wa mazingira katika maeneo ya makazi ya wananchi na sehemu za biashara na kuhakikisha wanazingatia mikataba yao ya kazi.

Shekimweri amesema Halmashauri hizo pia ziendelee kutumia kanuni na sheria ndogo ikiwemo kutoza faini ambazo zitawafanya watu wanaokikuka sheria za usafi wa mazingira kutozwa faini ambazo kwa mujibu kiwango ni kuanzia Shilingi 50,000 na zaidi na kwa kufanya hivyo itawafanya wananchi kutambua kuwa suala la usafi ni tabia ambayo inapaswa kuwa wajibu wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amesema katika kuelekea Kilele cha Siku ya Mazingira Duniani inayoadhimishwa kila tarehe 5 Juni mwaka huu, Tanzania imeendelea kuungana na Mataifa mbalimbali katika kutekeleza masuala muhimu yanayohusu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

“Kauli mbiu ya mazingira duniani mwaka mwaka 2023, inasema “Pinga uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki” Lengo la kauli mbiu hii inalenga kuondoa matumizi ya plastiki katika jamii zetu kama tunaoona katika eneo hili tunalofanya usafi na hivyo kuchangia katika uchafuzi wa mazingira” amesema Dk. Komba.

DKt. Komba amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti matumizi ya plastiki ikiwemo katazo la matumizi ya plastiki lililotolewa na Serikali mwaka 2019, ingawa wapo baadhi ya wafanyabiashara wachache wasio waaminfu wanaoingia na kusambaza bidhaa hizo kwa ajili ya matumizi ya vifungashio na vibebeo.

Settings