'Mikoko husaidia kutunza mazingira ya pembezoni mwa bahari'

Dec, 16 2024

Miti ya Mikoko inatajwa kuwa na faida kubwa kwenye fukwe ya bahari katika utunzaji wa mazingira ambapo husaidia kuzuia mmomonyoko wa fukwe kutokana na mawimbi ya bahari wakati wa bamvua kuu na dogo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga Bw. Twaribu Mkongo Aprili 16,2024 wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 ambapo amesema katika wilaya hiyo kuna aina tisa ya miti ya Mikoko.

Amesema wananchi wa eneo hilo pamoja na kazi nyingine lakini wamekuwa wakipanda miti ya Mikoko ikiwa njia ya kurejesha eneo linaloharibika kutoka na mmomonyoko wa ardhi.

“Mara nyingi tunatoa elimu ya namna ya kuhifadhi na kulinda mazingira pamoja na kufanya doria kupitia vikundi ambavyo vimeundwa na jamii yenyewe,” amesema Bw. Mkongo.

Kwa upande wake, Afisa Misitu Mwandamizi Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Timotheo Mande amesema Tanzania nzima kuna ukubwa wa hekta 158,000 ya eneo la miti ya Mikoko kuanzia pwani ya Tanga hadi Mtwara na kuna aina 10 ya mikoko.

“Pamoja na kazi nyingine ya miti hiyo pia husaidia kufyonza hewa ya Kaboni mara kumi ya misitu ya nchikavu na huzuia mmomonyoko wa udongo.”

Ameongeza kuwa faida nyingine ya miti hiyo katika utunzaji wa mazingira ni kuchuja takataka ngumu na takataka kemikali kuingia baharini.

Katika eneo hilo Ofisi ya Makamu wa Rais imejenga kingo ya Mto Pangani wenye urefu mita 950 ikiwa pamoja na kupanda Miti aina ya Mikoko na kupanga mawe kwa lengo la kupambana na Mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mmomonyoko wa fukwe.

Settings