Mhe. Majaliwa: Ulinzi wa mazingira ni moja ya vipaumbele vya Serikali

Jun, 30 2022

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema suala la kulinda na kuhifadhi mazingira limeendelea kuwa moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema hayo leo Juni 30, 2022 wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Alisema Rais Samia katika hotuba zake mbalimbali ndani na nje ya nchi, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa ustawi wa jamii yetu na kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu.

Pia, Waziri Mkuu alisema mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu ambazo siyo endelevu na rafiki wa mazingira zimekuwa zikichangia sana uharibifu wa mazingira nchini.

Alitaja shughuli hizo kuwa ni ukataji wa miti hovyo, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu.

Mhe. Majaliwa aliongeza kuwa jitihada za Serikali katika kuhifadhi mapori ni katika kulinda tunu zilizopo kwenye maeneo muhimu kama vile Loliondo, Ngorongoro, Selou, Ruaha na Katavi.

Settings