Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amewaongoza wajumbe wa Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo katika mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mazingira Prof. Peter Msoffe aliyewasili Ofisi hizo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Juni 28, 2025.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi, Mhandisi Luhemeja pamoja na mambo mbalimbali amemkabidhi jukumu la kuhakikisha biashara ya kaboni kupitia bahari inachukua nafasi na kuleta tija.
Alisema maeneo mbalimbali yakiwemo ya pwani ya bahari yamejaliwa kuwa na misitu ikiwemo mikoko ambayo inahitaji kutumiwa ipasavyo katika biashara ya kaboni.
Alimwomba Naibu Katibu Mkuu huyo kushirikana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika eneo la miradi ya kaboni kwa kuiunganisha na ajenda ya nishati safi ya kupikia hasa uhifadhi wa misitu.
Alisema Wizara hiyo imefanya vizuri katika kutekeleza maelekezi ya Serikali ya kwa shule zake kuanza kutumia nishati safi na kuachana na kuni na mkaa hatua ambayo imechangia kuacha kukata miti na kuihifadhi kwa ajili ya biashara ya kaboni ambayo inawaingizia fedha.
“Mazingira ni sehemu ya kuisaidia nchi, tunayo misitu mingi lakini hatuitumii ipasavyo hivyo mwaka mpya wa fedha unaaonza uwe wa mabadiliko tunahitaji fedha hizi kutokana na biashara ya kaboni kwani mazingira ni uchumi,” alisema.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe alisema suala la mazingira liko moyoni kwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo watendaji hao hawana budi kuendelea kuyalinda kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aliahidi kutoa ushirikiano akisema anatambua wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha anaisaidia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikia kulinda mazingira.
Pia, Prof. Msoffe alisema yuko tayari kupokea mawazo mapya ya ubunifu katika suala zima la hifadhi mazingira ambayo yatakuwa chachu katika maendeleo endelevu.
Itakumbukwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Prof. Msoffe ambaye ameapishwa leo Juni 28, 2025 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, aliteuliwa kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Bi. Christina Mndeme.