Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

VICE PRESIDENT'S OFFICE

News

​Mgodi wapewa siku 14 kudhibiti maji taka


Serikali imesema uwekezaji wowote ni lazima uzingatie Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni zake ikiwa ni pamoja kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwakuwa ni takwa la Kisheria.

Hayo yamesemwa leo Wilayani Mbinga na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande mara baada ya kufanya ziara ya kukagua migodi ya uchimbaji wa Makaa ya mawe ya Tancoal Ltd na Ruvuma coal.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Chande ametoa siku 14 kwa Mgodi wa Tancoal kudhibiti maji taka katika mabwawa yao pamoja na kudhibiti vumbi ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa maeneo ya jirani.

"Mazingira ndio uhai wetu, tuyatunze na tuyalinde kwa gharama yoyote ile" Chande alisisitiza.

Chande ameshuhudia ukataji wa miti kwa kiwango kikubwa katika migodi hiyo na kuwaagiza migodi yote miwili kuandaa mpango wa muda mfupi wa upandaji miti ili kurejesha uoto wa asili.

Aidha, Naibu Waziri Chande ameagiza migodi hiyo ya makaa ya mawe kuhakikisha wanaanda na kutekeleza mpango madhubuti wa kurejesha ardhi katika hali ya awali mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamiika ikiwa ni pamoja na kupanda miti kwa wingi.

"Upandaji miti uwe ni utamaduni wetu, hapa mgodini miti mingi imekatwa, wekeni mkakati wa kuirejesha kipindi cha mvua" Chande aliagiza.

Katika hatua nyingine Waziri Chande amemuagiza Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Kanda ya Kusini Bw. Jamal Baruti kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha masuala ya Uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira yanakuwa endelevu.

Akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Mbinga Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Aziza Mangosongo amesema jitihada na mikakati mbalimbali imechukuliwa katika kudhibiti vitendo vya uchafuzi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za uchimbaji wa madini kwa kufanya ufutiliaji na usimamizi wa mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Uchimbaji, uchakataji na uuzaji wa madini ya makaa ya mawe Wilayani Mbinga zilianza mwaka 2012 kupitia Kampuni ya TanCoal Energy Ltd na siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la Makampuni yanayojikita katika utafiti na uwekezaji kwenye sekta ya madini.