Makamu wa Rais, Mkuu wa USAID wafanya mazungumzo Marekani

Sep, 21 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) Bi. Samantha Power, Mazungumzo yaliofanyika Jijiji New York Nchini Marekani.

Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Rais ametaja juhudi mbalimbali zinazofanywa zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya afya hususani Afya ya mama na mtoto kwa kuanzisha programu mbalimbali za kuokoa Maisha ya Mama na mtoto kwa kushirikiana na wadau ikiwemo programu ya M- Mama. Amesema serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa afya katika kuboresha huduma za afya na kuongeza juhudi katika ujenzi wa miundombinu ya afya ikiwemo vituo vya afya pamoja na hospitali.

Makamu wa Rais ameishukuru serikali ya Marekani kwa kushirikiana na Tanzania katika kupambana na Uviko 19 kwa kutoa msaada wa dozi milioni5 za chanjo ya ugonjwa huo.

Amesema serikali imeweka mkazo katika kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka sera rafiki na kuunganisha taasisi zinazohusika na uwekezaji ili kuondoa urasimu kwa wenye nia ya kuwekeza Tanzania. Pia Makamu wa Rais ametaja juhudi zinazofanywa katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji pamoja na nishati ili kuwa na mazingira rafiki kwa wawekezaji.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Makamu wa Rais amekaribisha USAID kushirikiana na Tanzania katika kupata teknolojia rafiki ya mazingira itakayowezesha wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi na kijamii bila kuathiri mazingira.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Maendeleoya Kimataifa la Marekani (USAID) Bi. Samantha Power amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuunga mkono juhudi mbalimbali za mageuzi hususani katika sekta ya afya na kilimo.

Bi Samantha ameongeza kwamba shirika hilo linaiunga mkono Tanzania katika kuifanya kuwa tegemeo la upatikanaji wa chakula kwa kuwezesha kupatikana kwa mbolea ya gharama nafuu itakayosaidia kuinua sekta ya kilimo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameshiriki Mjadala uliobeba ajenda ya Demokrasia ulioandaliwa na Shirika la la Maendeleoya Kimataifa la Marekani (USAID) na kushirikisha wakuu wa nchi na serikali pamoja na wakuu wa mashirika ya kimataifa , mjadala uliofanyika kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA) Jijini New York nchini Marekani.

Katika majadiliano hayo , Makamu wa Rais amesema serikali ya Tanzania imeweka mkazo katika mageuzi ya kuimarisha uchumi na utawala wa kidemokrasia kwa kuhakikisha sekta binafsi inashiriki vema katika ujenzi wa taifa pamoja na kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kufikia maendeleo.

Makamu wa Rais yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Settings