Makamu wa Rais azindua malori ya utalii

Aug, 17 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango leo Agosti 17, 2022 amezindua na kukabidhi malori maalum 44 yenye thamani ya Shillingi billioni 14.77 kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyonunuliwa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW). Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro.

Akihutubia Viongozi, Maafisa, Askari na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukanda wa Kusini hususan ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege ndani ya Hifadhi pamoja na kutangaza ipasavyo eneo hilo ili kuendeleza utalii katika Ukanda huo.

Ameongeza kwamba mradi huo ukitekelezwa ipasavyo utasaidia kuongeza fursa kwa mwananchi, kwani unalenga kutoa ajira zaidi ya 40,000 kwa wakulima na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za ukanda wa Kusini,kuhamasisha kilimo cha kisasa na kuchochea sekta nyingine ambazo zinachangia ukuaji wa uchumi.

Dkt. Mpango ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wote wa utalii kwa ujumla, kuwa wabunifu katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini Tanzania. Amewasihi kuhakikisha wanaongeza maeneo ya kitalii ambayo yana ladha mbalimbali za kitalii na kuvitangaza. Amewaasa watoa huduma wa sekta binafsi kutumia fursa ya uwepo wa idadi kubwa ya watalii nchini kuwekeza katika kujenga hoteli katika hifadhi.

Aidha Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha maeneo yanayopimwa kwa ajili ya mashamba, miradi au makazi yasiwe njia za wanyama pori. Amesema kumekuepo ongezeko la malalamiko kuhusu watu kupewa mashamba na viwanja kwenye mapito ya wanyama na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi na hasara kubwa. Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa ,TANAPA na TAWIRI kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakaebainika kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mradi wa REGROW unatekelezwa katika vijiji 61 ambavyo vipo Jirani na hifadhi za kipaumbele ikiwa lengo kuu ni kuwapa faida ya uhifadhi wa maliasili muhimu kwa nchi hasa katika kuchangia katika uchumi wa nchi kwa ujumla na mtu mmoja mmoja.

Amesema Miongoni mwa faida watakazopata wakazi hao ni pamoja na ajira zitakazotokana na miradi watakayopendekeza wao wenyewe na pia mradi utatoa ufadhili wa masomo kwa vijana kutoka vijiji hivyo kuanzia vyuo vya ngazi ya kati kama VETA, Chuo cha Utalii (NCT), Chuo cha Ufugaji Nyuki (BTI) na Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi (PWTI) na Vyuo vya Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Sokoine pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Awali akitoa taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa ameiomba serikali kurudisha mpango wa ujenzi wa barabara iliolenga kupita nje ya hifadhi ili kusaidia kupunguza vifo vya wanyama vitokanavyo na ajali, kupunguza takataka zinazotokana na watumiaji wa barabara hiyo pamoja na uwepo wa geti la udhibiti litakalotumika kudhibiti wanaoendesha mwendokasi hifadhini.

Amesema mkoa unaendelea na juhudi za kutangaza utalii ikiwa pamoja na kuwaomba wadau wa utalii kuwekeza katika miundombinu ya malazi ili kuboresha sekta hiyo.


Settings