Makamu wa Rais aweka jiwe la msingi ujenzi Hospitali ya Wilaya Rombo

Jul, 18 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 18 Julai 2022 ameweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Ujenzi unaogharimu shilingi bilioni 7.9 ukiwa na jumla ya majengo 22.

Akihutubia mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo, Makamu wa Rais ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha awamu ya kwanza ya hospitali hiyo inakamilika mwezi wa tisa na kuanza kutumika kuanzia tarehe 1 Oktobamwaka huu.Makamu wa Rais amewataka viongozi na watoa huduma za afya katika hospitali hiyo kulinda vifaa, majengo pamoja na kuhakikisha dawa zinazopelekwa zinatumika kwa lengo lililokusudiwa na sio kuuzwa katika maduka ya dawa binafsi

Aidha Makamu wa Rais amezipongeza na kuzishukuru taasisi zote za dini zinatoa huduma mbalimbali kama vile afya na elimu kwa jamii na kuagiza Hospitali ya Huruma iliopo wilaya ya Rombo kuendelea kuwa na hadhi ya hospitali ya Wilaya.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Rombo pamoja na wananchi wote kwa ujumla kulinda na kuhifadhi vema mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi. Makamu wa Rais amewaagiza watendaji wa Serikali katika ngazi zote kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu ya mabadiliko ya tabianchi na mbinu bora za kilimo ambazo hazitasababisha uharibifu wa mazingira.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewahimiza wafanyabiashara wa Wilaya ya Rombo kufanya biashara kwa kufuata utaratibu na sheria zilizopo ikiwemo kupitia katika vituo rasmi vya mipaka. Amemtaka Mkuu wa Mkoakupitia baraza la biashara la mkoakutatua changamoto zote zinazojitokeza na kupelekea wananchi kutumia njia zisizosahihi katika ufanyaji biashara na nchi jirani.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Mhe. David Silinde amesema serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali za halmashauri 126 nchi nzima hadi kufikia juni 2022 pamoja na kutoa shilingi bilioni 13 ambazo zitatekeleza miradi ya ujenzi wa hospitali katika halmashauri 28 ambazo hazijawahi kuwa na hospitali tangu kupata uhuru.

Mheshimiwa Silinde ameongeza kwamba serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya ili kukabiliana na changamoto zilizopo ikiwemo vifaa tiba na nyumba za watumishi na uchakavu wa vituo. Aidha amesema Tamisemi imetenga shilingi bilioni 40.05 ili kuendeleza ujenzi wa hospitali 59 za halmashauri pamoja na bilioni 16.55 kukarabati hospitali kongwe za halmsahauri.

Awali akitoa taarifa za ujenzi wa hospitali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rombo Kanali Hamis Mahiga amesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wa Wilaya ya Rombo zaidi ya laki tatu. Ameongeza kwamba kukamilika kwa mradi huo kutapelekea kutoa huduma za kisasa kwa wagonjwa wa nje, kulaza wagonjwa, dharura kwa wagonjwa wote, upasuaji mkubwa, huduma bora za maabara pamoja huduma bora za afya ya mama na mtoto.

Settings