Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 18 Machi 2022 ametembelea na kukagua Shamba la Miti katika Msitu wa Rubare na maporomoko ya maji Kyamunene yaliopo Bukoba mkoani Kagera. Akiwa katika Msitu huo Makamu wa Rais amewataka viongozi wa mkoa wa Kagera kuendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti. Makamu wa Rais amesema msitu huo una mchango mkubwa kwa vyanzo vya maji vya mkoa huo hivyo ni muhimu kulindwa dhidi ya uharibifu wa mazingira. Makamu wa Rais amewaasa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kutoa elimu na utaalamu wa vijana wanaojishughulisha na shughuli hizo katika halmashauri zote nchini ili waweze kuendeleza ujuzi huo kwa wengine na kuchangia katika uhifadhi. Aidha Makamu wa Rais amesema ipo haja ya kuanza kuwatumia kikamilifu wanafunzi tangu wakiwa wadogo katika masuala ya uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwapa elimu pamoja na motisha za kutembelea vivutio vya utalii vya kimazingira wakati wanapofanya vizuri darasani. Pia Makamu wa Rais amewapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kutumia mvua zinazoendelea kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi. Awali akimkaribisha Makamu wa Rais katika shamba hilo Mkuu wa Uhifadhi Mandalo Salum amesema uanzishwaji wa shamba hilo umelenga kulinda vyanzo vya maji pamoja na mmomonyoko wa udongo ambapo katika msitu wa Rubare wenye jumla ya Hekta 6374 upandaji miti umefanyika katika hekta 2551 huku zinazobaki zikitumika kulinda vyanzo vya maji. Mandalo amesema shamba hilo limekua likichangia mapato ya serikali kuu kupitia uuzaji wa miti pamoja na kutoa asilimia tano ya mapato yake kwa serikali za mitaa. Aidha ameongeza kwamba tayari shamba hilo limechangia shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo ikiwemo kutoa madawati kwa baadhi ya shule wilayani Bukoba, ujenzi wa ofisi za vijiji, zahanati na maabara. Aidha amesema shamba la miti katika msitu wa Rubare litaendelea kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo pamoja na kuvutia watalii katika maporomoko ya maji ya kyamunene.
|