Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Vice President's Office

News

Makamu wa Rais ashiriki majadiliano mabadiliko ya tabianchi


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameshiriki majadiliano ya viongozi wa juu wa mataifa mbalimbali katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi katika Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea (LDCs) unaofanyika Doha nchini Qatar.

Akizungumza katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ametoa wito kwa mataifa kuhakikisha masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudhibiti uzalishaji wa gesi joto yanajumuishwa katika mipango ya maendeleo kwa kuzingatia sekta zilizo hatarini kukabiliwa na mabadiliko ya tabianchi kama vile nishati, kilimo na maji.

Aidha amesema ni muhimu kuongeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoyakabili mataifa kwa sasa na kuwekeza katika teknolojia bunifu zinazofaa katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na changamoto zinazohusiana ili kuwa na mweleko mzuri wa baadaye. Makamu wa Rais amesema maazimio yaliofikiwa katika mikutano iliopita ya mazingira ikiwemo ya Glasgow, Paris na Sharm El- Sheikh lazima yazingatiwe na kutoa wito wa kuzingatia haki kwa nchi za Afrika katika kuelekea katika matumizi ya nishati safi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania inakaribisha ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele ambayo yatasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile nishati ya jua na upepo, usimamizi bora wa taka pamoja na teknolojia rafiki kwa mazingira.

Awali Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametaja athari mbalimbali zilizoikumba Tanzania kutokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa kukiwa na matukio makubwa kama vile ukame na mafuriko, hali ya mvua isiyotabirika, kupanda kwa kina cha bahari na baadhi ya visiwa kuzama na kusababisha uhaba wa chakula, migogoro ya kijamii pamoja na kupanda kwa gharama za Maisha. Ameongeza kwamba Tanzania inakadiriwa kuwa na hasara ya kiuchumi hadi kufikia dola milioni 33.7 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kutokana na mafuriko.

Makamu wa Rais amesema katika kukabiliana na hali hiyo serikali inachukua hatua mbalimbali ikiwemo uchimbaji wa mabwawa kuhifadhi maji, kuhamasisha nishati safi ya kupikia, upandaji miti kila mkoa, kujenga kingo kando ya bahari kudhibiti mmomonyoko wa udongo, mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuandaa mpango kabambe wa mazingira wa mwaka 2022-2032.

Majadiliano hayo yalioshirikisha viongozi kutoka mataifa yalioendelea, wakuu wa taasisi binafsi pamoja na wakuu wa mashirika na jumuiya za kimataifa wito umetolewa wa kuunga mkono mataifa yanayoendelea kwa kufanyika mageuzi makubwa kuhakikisha urahisi wa upatitanaji fedha kufadhili miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea kwa kuzingatia madhara makubwayanayojitokeza kwa mataifa hayo yenye kiwango kidogo cha uchafuzi wa mazingira.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 07 Machi 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Slovenia Mheshimiwa Natasa Pirc Musar, Mazungumzo yaliofanyika katika Mji wa Doha nchini Qatar kando yaMkutano wa Tanowa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea (LDCs).

Viongozi hao wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za kimaendeleo pamoja na uhifadhi wa mazingira. Rais wa Slovenia ameikaribisha Tanzania kushirikiana katika kupata teknolojia rafiki kwa mazingira ambayo nchi hiyo imewekeza zaidi.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Fedha na MipangoDkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Saada Mkuya,Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki BaloziMbarouk N. Mbarouk pamoja na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa (New York)Balozi Dkt. Suleiman Haji Suleiman.

Makamu wa Rais yupo nchini Qatar kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea (LDC5).