Makamu wa Rais akutana na viongozi wa Ofisi yake na NEMC

Jun, 06 2020

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 6 Juni, 2020 amekutana na Viongozi na Watumishi Waandamizi wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika Kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage uliopo katika Jengo la Treasury Square, Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho ambacho ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayofanyika kila mwaka ifikapo tarehe 5 Juni, Mheshimiwa Makamu wa Rais amezungumzia tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha miaka mitano tangu aingie madarakani. Lengo ni kuona tunaposherehekea Siku ya Mazingira Duniani, Ofisi imekuwa ikisimamia vipi suala zima la uratibu wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kwa uendelevu. Kwa mfano, usimamizi wa miradi ya maendeleo inayolenga kurekebisha mifumo ikolojia na bioanuai, kupunguza gesijoto na kuhakikisha tunapanda miti ili kunyonya hewa ukaa, kupunguza ukame na kuhakikisha usalama wa chakula, kurekebisha mazingira katika migodi kwa kuhakikisha uoto wa asili unarejeshwa mara baada ya migodi hiyo kufungwa.

Aidha, Mheshimiwa Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Ofisi kuwa na takwimu na tathmini zinazoonesha uhalisia wa uchafuzi wa mazingira unaotokana na shughuli za binadamu. Kwa mfano; ukataji wa miti kiholela, uchimbaji wa mchanga na vifusi, utiririshaji wa maji sumu na maji taka kutoka kwenye migodi kwenda kwenye vyanzo vya maji, mito na maziwa.

Vile vile Mheshimiwa Makamu wa Rais ameelekeza kuwa, ili kuweza kuratibu kwa ufanisi shughuli za binadamu zinazochangia kwenye uharibifu wa mazingira kuna umuhimu wa kufanya mapitio ya Sera ya Mazingira ili kuja na mkakati utakaoainisha majukumu, changamoto na maono ya Ofisi kwa kushirikiana na sekta mbalimbali.

Ili kuhakikisha kuwa wananchi wanawajibika moja kwa moja katika utunzaji na usimamizi wa mazingira, Mheshimiwa Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kushirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha kuwa takwimu za mazingira katika sekta mbalimbali zinawekwa sawa kuanzia ngazi za chini. Aidha, Mheshimiwa Makamu wa Rais amepongeza hatua zilizochukuliwa na Ofisi katika usimamizi wa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.

Mheshimiwa Makamu wa Rais ameagiza Ofisi kwa kushirikiana na TAMISEMI kukamilisha mchakato wa kupatikana na kupewa mafunzo stahiki Wakaguzi wa Mazingira katika Halmashauri zote nchini.

Mheshimiwa Makamu wa Rais amewataka viongozi na watumishi kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa Reli ya SGR na Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere, ili kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu. Makamu wa Rais pia amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kushiriki vitendo vya ubadhirifu ambavyo vimekuwa vikiitia doa Ofisi.

Mwisho, Mheshimiwa Makamu wa Rais amesisitiza suala la kufanya tathmini katika maeneo yote ya migodi na wachimbaji wadogo ili kubaini kiwango cha uharibifu wa mazingira na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati kabla madhara kwa binadamu na mazingira hayajatokea. Amewataka viongozi na watumishi kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma ili kuongeza uelewa kwa wananchi katika masuala ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

Settings