Makamu wa Rais aelekeza viongozi kuchukua hatua kali kwa waharibifu wa mazingira

Apr, 02 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewaelekeza viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri kuwachukulia hatua kali za kisheria watakaokutwa na hatia ya kuharibu mazingira.

Ametoa maelekezo hayo leo tarehe 2 Aprili 2022 wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022, hafla iliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.

Alisema kuwa kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, upandaji miti, kupendezesha miji yetu na kufanya usafi ni lazima ziwe za kudumu.

Makamu wa Rais alitoa wito kwa wananchi wote kutunza mazingira na kutoa pongezi kwa wananchi wa Mji wa Njombe kwa kuwa mfano katika usafi mazingira miongoni mwa miji hapa nchini.

Aidha, Mhe. Dkt. Mpango aliwataka Taasisi ya Kupambana naKuzuia na Rushwa (TAKUKURU) kukamilisha uchunguzi wa miradi 52 iliyotiliwa shaka wakati wa mbio za Mwenge za Mwaka 2021 na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani haraka iwezekanavyo endapo kutakua na ushahidi wa kutosha.

Pia aliwataka wakimbiza mwenge kwa mwaka 2022 kuhakikisha wanajiridhisha endapo miradi watakayotakiwa kuizindua inalingana na thamani ya fedha iliyotumika, amewataka kufanya uchunguzi endapo watatilia shaka na hatua za sheria zichukuliwe.

Kuhusu suala la Sensa, Dkt Mpango, amewaelekeza viongozi wote na waratibu wa zoezi hilo kuwaandaa wananchi ili waweze kushiriki zoezi la Sensa kikamilifu. Halikadhalika amewaomba Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa dini na Viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kuwaelimisha na kuhamasisha wafuasi au wanachama wao kuhesabiwa.

Makamu wa Rais ametumia hadhara hiyo kuwasisitizia wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi, ugonjwa wa malaria pamoja na kuzingatia masuala ya lishe kwa maendeleo ya afya zao na uchumi kwa ujumla. Kuhusu suala la mazingira Dkt. Mpango amesema hali ya uhifadhi wa mazingira nchini bado si yakuridhisha hivyo kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, upandaji miti, kupendezesha miji yetu na kufanya usafi ni lazima ziwe za kudumu.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa tangu kuhasisiwa kwa Mbio za Mwenge, zimeendelea kudumisha uhuru, amani, mshikamano, uzalendo na umoja wa kitaifa. Aidha amesema mbio za mwenge zimekuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo – Zanzibar Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita, amesema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na MIchezo, itahakikisha kuwa mambo yote yaliyopangwa kwa ajili ya maslahi ya vijana yanatekelezwa.

Ujumbe mkuu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 umelenga Sensa ya Watu na Makazi chini ya Kaulimbiu isemayo, “Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa tuyafikie Maendeleo ya Taifa.”

Settings